30.2 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

BOT NA MKAKATI WA UTUNZAJI WA NOTI NCHINI

*Mkoa wa Kigoma waongoza kwa uchakavu wa noti

Na Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM


SUALA la kuhifadhi fedha hasa noti katika mazingira nadhifu, bado ni changamoto kubwa kwa Watanzania wengi hasa maeneo mbalimbali ya nchi yetu sehemu za pembezoni.

Kutokana na hali hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hulazimika kuziondoa kwenye mzunguko noti nyingi zilizochoka hasa zile ambazo zimekuwa kwenye mzunguko wa fedha wa kawaida.

Hata hivyo, pamoja na kila wakati kutoa noti mpya zenye thamani ya shilingi ya Tanzania, lakini kwa muda wa miezi sita hujikuta  kulazimika kuziondoa kwenye mzunguko kutokana na kuchoka sana, jambo ambalo huchangiwa na namna zinavyohifadhiwa.

Hata hivyo, BoT inakiri kwa kusema kuwa bado kuna  changamoto kwa Watanzania wengi katika kutunza fedha za noti hasa ya Sh 500 na 1000.

Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini, ambapo katika kutimiza jukumu hili, Benki Kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denomination) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini Mtwara kwenye mafunzo kwa wanahabari wa fedha, lengo lake ni kuwajengea uwezo wa kuandika taarifa sahihi na Meneja Msaidizi Idara ya Sarafu kutoka Benki Kuu Tanzania
(BoT), Abdul Dolla.

Anasema noti ya Sh 500 ndiyo inayochakaa zaidi kwani imechukua nafasi kubwa kwenye mzunguko wa fedha, jambo liloifanya BoT kutoa sarafu ya Sh 500, lakini kwa sasa noti ya Sh 1000 ndiyo iliyochukua nafasi kwenye mzunguko  kutokana kuwa ni noti ya chenji.

Anasema sababu ya fedha hizo kuchakaa haraka inatokana na kutumika zaidi kwenye mzunguko wa fedha hasa kwa kuzingatia kundi kubwa la wananchi ndio watumiaji wakubwa.

“Hii noti ya Shilingi 500 na 1000  zinatumika zaidi ukilinganisha na noti ya Shilingi 10,000 au 5,000. Ni fedha ambazo zipo kwenye mzunguko zaidi.

“Pia utunzaji wa fedha bado changamoto kubwa katika jamii na ndio maana zinachakaa mapema. Ukifuatilia zaidi utabaini hizi noti za Shilingi 500 wengi ambao wanazitumia hawazitunzi vizuri na wala hawazipeleki
benki,” anasema Dolla.

Anasema sababu nyingine ya fedha hizo kuchakaa haraka inatokana na ukweli uliopo  kwa Watanzania ambao wanatunza fedha zao benki hawazidi asilimia 14.

Kutokana na hali hiyo, anasema sehemu kubwa ya fedha inabaki mtaani na matokeo yake zinachakaa.
“Ujue fedha nayo ina umri wake wa kuishi ambapo kwa fedha za noti  zinaishi kati ya miezi sita hadi saba.
“Kazi yetu idara ya sarafu ni kuhakikisha tunapeleka fedha safi katika mzunguko na zile ambazo zimechakaa tunazisaga katika mashine maalumu,” anasema Dolla.

Kutokana na hali hiyo, alitoa ombi kwa Watanzania kuhakikisha wanatunza fedha hizo kwani Serikali inatumia gharama kubwa kuchapa fedha hizo, huku akifafanua  kuwa fedha ni moja ya alama  muhimu ya nchi yetu, hivyo lazima zitunzwe vizuri.

Alisititiza wananchi kutunza fedha zao benki kwani ni njia mojawapo ya kuzifanya fedha kuwa safi, huku akiwakumbusha wenye fedha zilizochakaa kuzipeleka benki ili zibadilishwe. Dolla anasema wao wamekuwa na utaratibu wa kuchukua fedha ambazo zimechakaa ambazo zinapelekwa BoT na kisha kuzichambua kwa vifaa
maalumu.

“Zile ambazo zitaonekana kuchakaa sana zitasagwa na zile ambazo zitakuwa bado kulingana na vigezo vyetu basi zitarudi kwenye mzunguko,” anasema Dolla.

Alipoulizwa iwapo wamefanya utafiti kubaini mikoa ambayo inaongoza kwa wananchi kutumia fedha zilizochakaa, Dolla anasema kuwa Mkoa wa Kigoma ni moja ya mkoa ambao unaongoza kwa kuwa na fedha zinazoonekana kuchakaa haraka kwenye mzunguko.

Anasema sababu mojawapo inayoonesha bado wananchi walio wengi hawana mwamuko katika kutunza fedha na pia miundombinu ya usafiri ndani ya mkoa huo inachangia fedha zinazochakaa huchelewa kusafirishwa ili zibadilishwe.

Kuhusu sarafu ya senti kurudishwa kwenye mzunguko, Dolla anasema siku za karibuni swali hilo lilijibiwa vizuri bungeni, ila kwa kuongezea ni kwamba sarafu za senti bado zipo na ndio maana kwenye vitabu vya benki
zipo.
Anasema hata BoT haijatangaza kutozitambua senti ila kinachotokea ni  nguvu ya soko katika kununua.
“Noti ya Shilingi 500 hupita kwenye mikono ya watu wengi zaidi na ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida, hivyo kuchakaa haraka ndio maana tumeamua kutoa toleo la sarafu,” anasema.

Akifafanua zaidi, Dolla anasema sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti na pia noti zimekuwa zikikaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati mwafaka ili
zibadilishwe.
Akitaja sifa za sarafu hiyo mpya ya Sh 500, Dolla anasema kwanza umbo lake ni la duara lenye michirizi pembezoni na kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5.

“Sifa nyingine ni kuwa ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma na Nickel na kwa upande wa mbele ina sura ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani,” anasema Dolla.

Aidha, anabainisha kuwa sarafu hiyo kwa upande wa nyuma ina kivuli kilichojificha ambacho huonesha thamani ya sarafu ya 500 au neno BoT inapogeuzwa geuzwa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles