Na Mwandishi Wetu
OFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema tofauti na zamani, kwa sasa fani ya ununuzi na ugavi ni nyeti kitaasisi na muhimu katika mafanikio ya biashara za kisasa.
Kwa mantiki hiyo amewataka wataalamu wa ununuzi na ugavi nchini kuzingatia maadili, uadilifu na weledi katika sehemu zao za kazi.
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini (APSP) uliofanyika Jumanne Novemba 30,2021, jijini Arusha ambapo alikuwa mgeni rasmi, Zaipuna amesema mabadiliko ya kisheria yamewafungulia fursa mpya wataalamu hao.
“Nina imani kuwa mtatumia mkutano huu kujadili, kuchambua na kuweka mikakati ya uboreshaji katika fani ya manunuzi na ugavi…nia ikiwa ni kuongeza uadilifu, uaminifu na ufanisi kwenye sehemu zenu za kazi,”amesema Zaipuna.
Aidha, amewataka wataalamu hao kuweka sawa uwiano kati ya mahitaji ya biashara na miongozo ya sheria na kanuni za manunuzi ili waendane na kasi ya mabadiliko na mahitaji kwenye maeneo yao ya kazi.
Baada ya kutoa nasaha hizo, alizindua Bima ya Maisha ya Mkono wa Pole kwa ajili ya wanataaluma wa fani ya Ununuzi na Ugavi na kuwashukuru s wana APSP kwa kujiunga na utaratibu huo wa NMB wenye lengo la kuwasaidia wanapokumbwa na janga la kifo.
Naye Mwenyekiti wa APSP, Emmanuel Urembo, aliipongeza NMB kwa kuwa kinara wa huduma za kifedha nchini akisema hilo linadhibitishwa na kupata kwake tuzo nyingi za kimataifa za ubora na ufanisi katika shughuli zake.
Amesema umuhimu wa chama chao na thamani ya tasnia hiyo unatokana na ukweli kuwa takribani asilimia sabini ya fedha zinazotengwa kwenye bajeti ya serikali na taasisi binafsi zenye miradi ya maendeleo hutumika kwenye ununuzi wa vifaa, huduma, kazi za ushauri na ujenzi.
“Hivyo, kuanzishwa kwa APSP ni habari njema katika kuhakikisha kwamba usimamizi bora wa mnyororo wa ununuzi na ugavi wa umma na utunzaji vifaa unazingatiwa wakati wote katika kuhakikisha jamii inapata thamani bora ya fedha zinazotumika,”amesema.
Urembo ametahadharisha kuwa kwa kutowatumia wataalamu wenye weledi, maarifa na nidhamu taasisi nyingi zitaendelea kuwa kwenye hatari ya kupoteza fedha nyingi katika eneo la ununuzi na ugavi.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ununuzi na Ugavi (CIPS), swala la maadili na uadilifu linazidi kuwa nyeti kutokana na kuimarika kwa hadhi ya fani hiyo.