24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

BOSI MAGEREZA AIBUA MASWALI

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP), John Minja
Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP), John Minja

Na EVANS MAGEGE – Dar Es Salaam

KITENDO cha Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP), John Minja, kuomba kusitisha mkataba wake wa kazi na kustaafu, kimeibua maswali makuu matatu.

Maswali hayo, likiwamo kwanini aliomba kustaafu licha ya kwamba aliongezewa muda, yameibuka ikiwa ni siku moja tu tangu Rais Dk. John Magufuli aridhie ombi lake.

MTANZANIA Jumapili limebaini maswali hayo kupitia hoja zinazovuma katika mijadala mbalimbali ya kijamii, huku kubwa likiwa ni lile linalohoji sababu ya msingi iliyomsukuma Minja kumwomba Rais Magufuli asitishe mkataba wake.

Swali jingine lililoibuka baada ya uamuzi huo ni lile la kutaka kujua ni lini alipeleka maombi yake, kwamba ilikuwa kabla au baada ya Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga.

Katika muktadha huo, swali la tatu lililoibuka ni lile linalohoji muda aliotumia Rais Magufuli kuridhia ombi la Minja.

Kutokana na maswali hayo, juzi na jana MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Minja kwa simu ya kiganjani ili ayatolee ufafanuzi, lakini haikupokewa kila ilipopigwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.

Pia MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, ili kupata majibu ya maswali hayo, ikiwamo sababu aliyoeleza Minja ya kutaka kustaafu na kusitishiwa mkataba wake, na kama barua hiyo aliiandika baada ya Magufuli kutembelea Gereza la Ukonga.

Katika majibu yake, Msigwa mbali na kukiri Minja aliwahi kuongezewa muda kwa sababu umri wake wa kustaafu ulishafika, lakini hakuweza kujibu maswali hayo.

“Sijui kama aliandika barua hiyo baada ya Rais Magufuli kutembelea Ukonga na katika barua yake aliiomba kusitisha mkataba wake na kustaafu na amekubaliwa kama taarifa ya jana (juzi) ilivyosema,” alisema Msigwa.

Uamuzi wa Minja kuomba kusitisha mkataba na kuibua maswali hayo, umekuja baada ya Rais Magufuli Jumanne ya wiki hii kufanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga.

Katika ziara yake hiyo, Rais Magufuli alibaini kasoro kadhaa zinazolikabili Jeshi la Magereza, ikiwamo askari kuuziwa sare za jeshi kutoka kampuni za watu binafsi.

Rais Magufuli alisema kitendo cha askari hao kununua sare za kazi kwa watu binafsi ni kinyume na taratibu za majeshi nchini.

Akizungumza na askari magereza katika ziara hiyo, Magufuli alipiga marufuku watu binafsi kuuza sare za majeshi, huku akiwataka wale wote wanaoziuza wazikabidhi kwa majeshi husika mara moja.

Magufuli alipiga marufuku hiyo kutokana na maelezo kutoka kwa baadhi ya askari magereza, kuwa wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi kinyume na taratibu.

Kutokana na maelezo hayo, Magufuli alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi ya hapa nchini.

Pia alipiga marufuku majeshi yote nchini kuingia ubia na watu binafsi kupangisha ama kuuza maeneo yao kwa kufanya biashara na kutaka maeneo yote ya majeshi yabaki katika jeshi husika.

Haiwezekani sare za majeshi yetu kuuzwa na watu binafsi, hilo haliwezekani kamwe, labda baada ya kumaliza muda wangu,” alisema Magufuli.

Mbali na onyo hilo, pia alitoa Sh bilioni 10 kwa Magereza ili kujenga nyumba mpya zitakazotumika kwa makazi ya askari wake wanaoishi Ukonga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles