Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, ametoa taulo za kike kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma Shule za Sekondari za Ilala, Minazi Mirefu na Majani ya Chai ili kuwawezesha kuhudhuria masomo wakati wote bila ya kikwazo cha kukosa taulo.
Akizungumza Aprili 6, 2022 kwa niaba ya mbunge huyo ambaye yuko bungeni Dodoma, Katibu wake Lutta Rucharaba, amesema wana mkakati wa kutatua changamoto ya taulo za kike kwa wanafunzi kwani wengi wanatoka kwenye mazingira duni hali inayosababisha kushindwa kumudu gharama za taulo hizo na kukosa masomo.
“Mheshimiwa mbunge anakumbuka mazingira aliyokuwa anasoma hivyo aliona analo jukumu la kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa shuleni wakati wote. Tunafanya jitihada kuwafikia watoto wote wa kike ili wasikatishe masomo kwa sababu ya kukosa taulo za kike,” amesema Lutta.
Kwa mujibu wa Lutta tayari wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari jimboni Segerea wamepatiwa taulo za kike na kwamba wanatarajia pia kupeleka Shule za Sekondari Binti Mussa na Vingunguti.
Mmoja wa wanafunzi waliopatiwa taulo hizo anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Majani ya Chai, Aisha Rashidi, amemshukuru mbunge huyo kwa msaada huo kwani hedhi imekuwa ikisababisha baadhi yao kukosa masomo kwa sababu ya kukosa taulo za kuvaa.
“Tunamshukuru sana mheshimiwa mbunge tumetambua kuwa kuna watu wengine wanatufikiria na kutukumbuka na hii itakuwa chachu ya sisi kuendelea kufanya vizuri katika masomo yetu,” amesema Aisha.
Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Perpetualmaterials inayotengeneza taulo za kike zijulikanazo kama ‘Girlpro’, Salma Muya, amesema wameguswa kushirikiana na mbunge huyo kutatua changamoto zinazowakabili watoto wa kike na kuahidi kuwa wataendelea kutoa kwa shule mbalimbali zikiwemo na za binafsi pia.
Aidha amesema watakuwa wakitoa zawadi kwa wanafunzi watakaofanya vizuri kwenye masomo na michezo katika shule mbalimbali ili kuinua kiwango cha taaluma.