Na RAMADHANI MASENGA
KATIKA mtandao maarufu wa WhatsAap niko katika makundi mawili yanayohusu sanaa. Moja limejaa wasanii maarufu wa Bongo Muvi na lingine limejaa wasanii maarufu wa Bongo Fleva.
Katika kundi la Bongo Fleva wasanii wanajadiliana, wanasifiana na wanahamasishana kufanya kazi nzuri. Kwao sio aibu msanii kusema tuige mfano wa msanii fulani ama sio hatari kusema Vanesa Mdee katika kipindi kifupi cha sanaa yake kafanya mambo makubwa ambayo wakongwe wengi waliishia kuyaota.
Namna wasanii wa Bongo Fleva wanavyoishi, sio ajabu kwa sanaa yao kuwa hivi. Hata upinzani wa Diamond na Ali Kiba ulivyo, wenyewe wanaufanya kibiashara zaidi ndiyo maana nyimbo za magwiji hawa zikitoka huzua gumzo kubwa mtaani.
Unakumbuka kisanga cha Seduce Me na Zilipendwa? Japo kuna ‘ujanja ujanja’ mwingi katika kuvutia mashabiki wao, ila hiyo haiondoi ukweli kwamba wanajua nini wanachofanya. Shida iko katika Bongo Muvi.
Japo sanaa hiyo bado imesinzia ila kila msanii anajiona anajua kuliko mwingine na ana uwezo wa kuzungumzia uwezo na kazi za wengine.
Japo sio rasmi ila Bongo Muvi imejigawa katika makundi mawili. Kati ya wasanii wa zamani na wasanii wa kizazi kipya. Wasanii wa kizazi kipya hujifanya wanajua zaidi kuliko wa zamani.
Kwa kujifanya huku, basi wasanii wakongwe na wenyewe wanataka kuwaonesha madogo kwamba hawawezi kitu na kuwafanyia vigisu ili waonekanae sio mali kitu. Jitihada hizi zote hazina mchongo katika maendeleo ya sanaa yao ilifubaa.
Katika hali ya kushangaza, niliona baadhi ya wasanii wa kizazi kipya cha filamu wakiona hata suala la mchango wa fedha kwa ajili ya matibabu ya msanii Wastara Juma haliwahusu sana. Ni ujinga mkubwa.
Uhayawani mwingine uliopo katika kundi la Bongo Muvi ni siasa. Eti kwa sababu fulani anashabiki chama fulani, basi wengine wasioshabikia chama hicho wanajiona hawastahili kufanya kazi ama kushauriana na mwenzako. Ni ujinga.
Bongo Fleva hakuna mauzauza haya. Inajulikana Ney wa Mitego ni Chadema na Diamond ni CCM ila wanashirikiana na kukubaliana kazi zao vizuri. Inajulikana kina Said Fella, Babu Tale ni CCM, ila Roma wakihitaji msaada wanasaidiwa na wadau hao.
Huu ndio ukomavu unaohiotajika kwa watu. Kama mnaweza kubaguana kwa sababu ya itikadi zenu za vyama, baadaye itashindikana vipi kubaguana kwa sababu ya dini na makabila yenu? Mambo ya ajabu kabisa haya.
Ujuaji ulipo Bongo Muvi utazidi kuidumaza sanaa hiyo kuliko kuiendeleza. Kuna msanii mmoja wa kawaida tu ila sasa anaona udhia kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kunusuru sanaa hiyo eti kisa yeye yuko chama cha upinzani. Utoto wa hali ya juu.
Ushabiki na kazi ni vitu viwili tofauti. Mtu makini na mwenye kujua anachofanya hawezi kushabikia chama zaidi kuliko kuithamini kazi yake. Hao wanasiasa, siasa kwao ni kazi.
Vipi wewe unayeacha kushabiki kazi yako na kushupalia ya mwenzako? Wasanii Bongo Muvi mbadilike.