26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Bomu la tano latua, lajeruhi tena Arusha

Majeruhi wa bomu la mkono Arusha
Majeruhi wa bomu la mkono Arusha

Eliya Mbonea na Abraham Gwandu, Arusha

KIONGOZI wa Taasisi ya Answaar Muslim Youth Centre Kanda ya Kaskazini, Sheikh Sudi Ally Sudi, amejeruhiwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Majengo jijini Arusha.

Aidha, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, Muhaji Hussein (38), alipatwa na mkasa huo akiwa nyumbani kwa Sheikh Sudi akitokea safarini Nairobi, Kenya.

Katika mkasa huo, Muhaji alivunjika mguu wa kushoto na kukatika vidole vitatu vya mguu wa kulia kutokana na mlipuko huo.

Ilielezwa kwamba, watu wasiojulikana walivunja kioo cha dirisha usiku huo kisha kurusha bomu hilo hadi sehemu walipokuwa wamekaa watu hao.

Hata hivyo, familia ya Sheikh Sudi imesalimika kutokana na kuwa katika chumba kingine ambacho hakikuathiriwa haraka na mlipuko huo.

Akizungumza katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru alipolazwa, Sheikh Sudi alisema tukio hilo lilitokea wakati wakiwa wanajiandaa kula daku akiwa na mgeni wake, Muhaji.

Sheikh Sudi akizungumza kwa taabu kitandani alipolazwa katika wodi ya majeruhi alidai kabla ya tukio la bomu tayari alishaanza kupokea vitisho vya kupoteza maisha ikiwamo kutishiwa kwa risasi.

“Nimetishiwa mara kadhaa kabla ya tukio hili nilisharipoti katika vyombo vya dola, ila wameniumiza sana bila sababu,” alisema Sheikh Sudi.

Majeruhi mwingine Muhaji ambaye ana majeraha makubwa maeneo yake ya miguu kuanzia chini ya magoti alisema anamshukuru Mungu kwa kumlinda katika tukio hilo.

“Hapa nilipo nimepata majeraha makubwa katika miguu yote miwili, ambapo mguu wa kushoto umevunjika na mguu wa kulia kidole gumba na vidole viwili vinavyofuata vimekatika,” alisema Muhaji na kuongeza:

“Kabla ya mlipuko mwenyeji wangu alikuwa anasimulia jinsi anavyopokea vitisho wakati huo mtoto wake alikuwa akiandaa chakula.

“Bahati mzuri mtoto alikuwa ameshamaliza na kuondoka tulipokuwa ndipo nikasikia kishindo cha kuvunjwa kioo cha dirisha kilichofuatiwa na mlipuko,” alisema.

DAKTARI WA ZAMU

Kwa upande wake daktari wa zamu katika wodi ya majeruhi, Leo Temba, alisema hali za majeruhi wote wawili inaendelea vizuri na tayari walishawapatia huduma zote muhimu.

Akimzungumzia Muhaji alisema ndiye majeruhi aliyekuwa na hali mbaya zaidi kutokana na kuvuja damu nyingi, hata hivyo baada ya kupatiwa matibabu anaendelea vizuri.

“Wagonjwa wangu mpaka wakati huu wanaendelea vizuri, tumefanya jitihada kuokoa maisha yao. Tumewaongeza damu hasa Muhaji.

“Wote tumesafisha vidonda na kuondoa mabaki yote ya chumachuma na kufunga vidonda ili kuepusha damu kuvuja kwa wingi.”

“Muhaji ndio yuko ‘serious’ amevunjika mguu wa kushoto na una vidonda vikubwa ambavyo tumevifunga na tutavishona. Lakini pia mguu wa kulia umeumia kwani vidole vitatu vimekatika, gumba na vidole viwili vya katikati,” alisema Dk. Temba.

MKUU WA MKOA

Akiwa hospitali kuwatembelea majeruhi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa uchunguzi wa awali umebainisha mlipuko huo hauna uhusiano wowote na vikundi vya kigaidi vya Al- Qaeda wala Al- Shabaab.

Magessa alisema kwamba upo mgogoro baina ya waumini wa taasisi za dini ya Kiislamu katika Msikiti wa Qiblatein Kandahari eneo la Soko la Kilombero jijini Arusha.

“Lipo tatizo la ndani kati ya waumini wa Kiislamu kwani Sheikh Sudi ametuambia tayari alishapokea vitisho kutokana na kukataa kutumiwa kwa msikiti huo na makundi ya siasa kali yanayoongozwa na Answar Sunna.

“Tunaendelea kuwasaka vijana hawa tutawakamata wote na kuwafikisha mbele ya vyombo ya sheria,” alisema Mulongo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, akizungumzia tukio hilo akiwa Hospitali ya Mount Meru alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema Jeshi la Polisi litahakikisha linawakamata watuhumiwa wote.

“Pale msikitini kuna msuguano mkali kati ya waumini wenye msimamo mkali na wasio na msimamo mkali. Tupo kazini kuwasaka wote waliohusika na kitendo hiki,” alisema Kamanda Sabas.

Kutokea kwa tukio la Sheikh Sudi kurushiwa bomu akiwa nyumbani kwake linakuwa tukio la tano linalohusiana na matukio ya ulipuaji wa mabomu jijini Arusha.

Tukio la kwanza la mlipuko wa bomu kutokea jijini Arusha lilikuwa ni katika Kanisa la Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,Olasite, kisha kufuatiwa na mlipuko wa bomu la nyumbani kwa Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha.

Baada ya hapo mlipuko mwingine wa bomu ulitokea kwatika mkutano wa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), viwanja vya Soweto kisha kufuatiwa na mlipuko wa bomu katika Bar ya Arusha Night Park (a.k.a Matako Bar).

Mlipuko mwingine sasa unakamilisha idadi ya milipuko mitano ya mabomu kutokea jijini Arusha ni huu wa juzi ambapo Sheikh Sudi na mgeni wake wakiwa nyumba usiku walirushiwa bomu lililowajeruhi miguuni.

Kutokea kwa milipuko yote hiyo kulisababisha kupoteza kwa uhai wa watu ambao jumla ya watu tisa walipoteza maisha yao kutokana na milipuko hiyo huku majeruhu wa milipuko yote wakifikia zaidi ya 120,  ambao kwa nyakati tofauti walikuwa wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles