26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

BOB WINE ATEMA CHECHE

WAKISO, UGANDA


HATIMAYE Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi ambaye ni mwanamuziki maarufu anayefahamika kwa jina la Bob Wine, amewaambia ukweli wananchi juu ya mkasa uliomkuta katika kampeni za uchaguzi mdogo huko Gulu, kuangukia mikononi mwa vyombo vya dola na kisha kulazimika kusafiri kufuata matibabu zaidi nchini Marekani.

Bob Wine ambaye juzi alilazimika kutii amri ya Jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege jijini Entebbe akitokea Marekani, ambapo jeshi hilo lililazimika kumzingira na kumlinda pamoja na kumsindikiza hadi nyumbani kwake Magere, katika Wilaya ya Wakiso, licha ya maelfu ya wafuasi na mashabiki wake kutalamaki katika viunga vya uwanja huo.

Akizungumza na maelfu ya wafuasi waliofurika nyumbani kwake Magere, katika Wilaya ya Wakiso nchini Uganda, amesema mara baada ya kuwasili uwanja wa Ndege wa Entebbe alikamatwa na watu wenye sare za Jeshi la Polisi na wengine waliovalia kiraia.

“Wakati nawasili uwanja wa ndege Entebbe leo (juzi), nilikamatwa na watu wenye sare za Jeshi la Polisi na wengine walivaa kiraia. Walininyang’anya fimbo yangu na kunilazimisha kuingia kwenye gari la polisi lililokuwa linanisubiri,” alisema Bob Wine na kuongeza:

“Nakushukuruni nyote kwa kufika hapa nyumbani kwangu Magere. Nakosa maneno mengi ya kuwashukuru. Namshukuru Mungu pia kwa kuniwezesha kurudi nyumbani nikiwa salama.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Uganda, kumekuwa na shamrashamra kubwa katika Kijiji cha Magere na maeneo mengine ya jirani.

Awali kulikuwa na taharuki katika majiji ya Kampala na Entebbe baada ya polisi kuzuia maandamano na kuwakamata watu wote wakiwemo waandishi wa habari.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Meya, Erias Lukwago pamoja na watu wengine kuzuiwa kutotoka nje kwa madai wanaweza kusababisha matatizo jijini humo.

“Kwa mara nyingine tena haki zangu zimevunjwa, lakini muhimu zaidi ni haki za rafiki zangu, familia yangu na wanasheria ambao wamedhalilishwa sana. Mashabiki wangu wengi wamekamatwa na wengine wameachiliwa huru,” alisema Bob Wine.

Ameongeza kwa kusema: “Nimewaona watu wengi waliokuwa wakienda kwenye shughuli zao kandokando ya barabara ya Entebbe na Kasangati, wakikamatwa na wengine kuzuiwa kuendelea na safari zao na baadhi ya wana usalama. Huu ni ukiukwaji wa sheria, unapaswa kuachwa mara moja.”

Awali, akizungumza na Shirika la habari la AFP, mke wa Bob Wine, Barbie Kyagulanyi, alisema: “Mara baada ya kuwasili katika mji wa Entebbe, vikosi vya usalama vilimzingira na hatujui vimempeleka wapi. Hatukuwa na taarifa ya sehemu alikopelekwa, kulikuwa na wasiwasi mwingi.”

Hata hivyo, mkuu wa Jeshi la Polisi la Uganda, Okoth Ochola, hata hivyo alisema Bob Wine alipelekwa nyumbani kwake na wala hakuwa kizuizini.

Mwanasheria wake, Robert Amsterdam, aliandika katika ukurasa wa kijamii wa Twitter kwamba mteja wake alikamatwa na maofisa wa kijeshi kinyume cha sheria.

Mapema nduguye Wine Eddy Yawe na Naibu msemaji wa chama cha Democratic Party, Waiswa Alex Mufumbiro, walikamatwa na vikosi vya usalama na kuzuiwa kwenye kituo cha polisi Uwanja wa Entebbe.

Msemaji wa polisi mjini Kampala, Luke Owoyesigyire, alionya kuwa yeyote ambaye angeshiriki kwenye shughuli yoyote inayomhusu Bobi Wine angekamatwa

Bob Wine aliondoka Uganda Agosti 31, mwaka huu kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kupata matibabu baada ya kupigwa na kuumizwa vibaya na maofisa wa polisi.

Tangu kuchaguliwa kwake katika Bunge mnamo mwaka 2017, Kyagulanyi, mwenye umri wa miaka 36, ameibuka kama msemaji wa vijana na mkosoaji mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, madarakani tangu mwaka 1986.

Kyagulanyi alikamatwa na kufikishwa baadaye mbele ya mahakama ya kijeshi huko Gulu kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria, lakini mahakama ya kijeshi ilifuta mashtaka hayo.

Hata hivyo, alikamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya uhaini kwa madai ya kuhusika katika vurugu za kurushiwa mawe msafara wa Rais Yoweri Museveni. Amekana madai hayo lakini atapanda kizimbani mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Bobi Wine, ameapa kuendelea kupigania uhuru nchini humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles