PALMAS, HISPANIA
ALIYEWAHI kuwa kiungo wa AC Milan na timu ya taifa ya Ghana, Kevin Prince Boateng, amethibitisha jinsi alivyoshindwa kukabiliana na umaarufu wa kuwa mwanasoka tajiri wa kulipwa baada ya kutumia vibaya fedha zake kwa kununua magari, kustarehe na marafiki wanafiki.
Boateng anayechezea Las Palmas ya nchini Hispania, alipata umaarufu huo akiwa anaichezea AC Milan.
Akizungumza na jarida la Marca la nchini humo, Boateng alisema hali hiyo ilimuathiri sana kwa kutumia fedha zake bila mpangilio wowote kwa sababu alikuwa na fedha nyingi inayoweza kununua chochote.
“Katika miaka miwili, nilitumia fedha yote kununua magari ya kifahari, saa za gharama, viatu, kwenda kustarehe usiku, mahotelini nikiwa na marafiki ambao naamini sikustahili kuwa nao.
“Nilikulia katika kitongoji masikini na nisiyekuwa na fedha, ilikuwa hatari, katika maisha ni bora ukatambua mabaya. Asante kwa makosa niliyoyafanya, kwa sababu ndiyo yaliyosababisha leo mimi kuwa hivi,” alisema Boateng.
Kustaafu
Mnamo Novemba 2011, Boateng alitangaza kustaafu kuichezea nchi yake ya Ghana akiwa na umri wa miaka 24 na hivyo kuzikosa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2012.
Septemba mwaka 2012, aliyewahi kuwa strika wa Marseille na timu ya taifa ya Ghana ambaye ni rafiki yake wa karibu, André Ayew, alithibitisha kuwa Boateng alikuwa na mpango wa kurejea kikosini lakini alishindwa kwenda kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2013.
Kombe la Dunia 2014
Tarehe 2, June 2014, Boateng alitajwa kwenye kikosi cha Ghana kilichoshiriki fainali hizo. Katika mechi ya ufunguzi aliingia kipindi cha pili dhidi ya Marekani na kufungwa mabao 2-1. Alicheza tena dhidi ya Ujerumani anayoichezea kaka yake Boateng.
June 26, Boateng akiwa kikosini alirejeshwa nyumbani kwa makosa ya utovu wa nidhamu saa chache kabla ya mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya Ureno.
Sababu inaelezwa kuwa alimkaripia kocha wake wa timu ya taifa, James Kwesi Appiah, wakiwa kwenye mkutano. Boateng pamoja na kiungo mwenzake, Sulley Muntari, walirejeshwa nyumbani. Na June 29, mwaka huo huo, Boateng alikikashifu Chama cha Soka nchini Ghana na kuwaeleza kuwa wanafanya mambo yao kitoto.