Sharifa Mmasi,Mtanzania Digital
KATIBU Mkuu wa Baraza la Michezo Zanzibar (BMTZ), Suleiman Koleza amesema kwa sasa visiwani humo hakuna uongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu (BAZA) hadi hapo mipango itakapo kamilika ili uchaguzi mkuu ufanyike.
Ikumbukwe kuwa BAZA ilitakiwa kufanya uchaguzi wake Julai 16 mwaka huu lakini haikuwa hivyo badala yake, viongozi mbalimbali wakiwemo wa BMTZ walikutana katika mkutano mkuu kujadili mambo mbalimbali ikiwamo suala la uchaguzi ambapo, mwafaka ulikuwa ni kupewa miezi kadhaa kupisha maandalizi.
Wakati maandalizi yakisubiriwa ili uchaguzi mkuu utangazwe, yaliibuka mapya siku tatu nyuma ikidaiwa kuwa, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita ameuvunja rasmi uongozi wa BAZA uliyopo madarakani kutokana na kuendesha mambo kinyume na Katiba inavyosema.
Baada ya hayo, uongozi wa BAZA ukatangaza hadharani kujitoa madarakani huku, mengi yakizungumzwa ikiwemo kumlaumu Waziri huyo kwamba, amefanya maamuzi kwa mihemko na jazba.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo kwa simu, Suleiman amefafanua : ” Ni kweli kwa sasa BAZA haina viongozi hadi hapo uchaguzi mkuu utakapo fanyika.
” Siwezi kusema rasmi ni lini uchaguzi utafanyika ila ninachojua ni kwamba, tupo kwenye maandalizi kuelekea uchaguzi lakini kwa sasa kila kitu kinachohusu mpira wa kikapu Zanzibar ikiwamo mashindano yamesimama,” amesema.