23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Biteko: Tumechoka kuhubiri injili, ukikamatwa unafutiwa leseni

Na Janeth Mushi, Arusha

Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema kuanzia sasa atakayekamatwa akitorosha madini ya Tanzanite,akikamatwa ataeleza ametoka mgodi gani na mmiliki wa mgodi huo atafutiwa leseni.

Aidha, amesema wanunuzi wadogo na wakubwa wa madini, wakikamatwa wanatorosha madini au kutumia vibaraka kutorosha madini,watafutiwa leseni zao na kutozwa faini ya Sh milioni 50 kama ambavyo Sheria inaelekeza.

Biteko ameyasema hayo leo Desemba 17, wakati akizungumza na wachimbaji wa madini hayo pamoja na wadau wengine wa madini katika eneo la ukuta wa Mirerani,wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara.

Amesema licha ya serikali kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji wa madini ikiwemo kufuta kodi zenye maudhi lakini bado baadhi yao wanaendelea kutorosha madini hayo.

“Haitakuwa rahisi tena Tanzanite kutoka hapa anayedhani anaweza kufanikiwa ajiandae kushindwa,nimekuja kuwaambia ujumbe huu,” amesema Biteko.

Biteko (pichani) amemwagiza Kaimu Afisa Madini mkoa wa kimadini wa Mirerani, Fabian Mshai kuandika barua kwa wamiliki wa migodi kuwa kuanzia sasa kazi ya ukaguzi wa madini itakuwa chini ya mameneja wa migodi.

“Akikamatwa mtu getini,tutakwenda kwa mwenye mgodi na hakuna adhabu nyingine ni kufuta leseni.Kila mtu amlinde mwenzake na hili sitanii Chunya nimefuta leseni 

“Unichukie unipende itakuwa hivyo na kuanzia leo imekuwa hivyo weka utaratibu kwenye mgodi wako mkague mwenyewe hii itasaidia. Injili ya kuhubiri tumechoka kuanzia leo atakayekamatwa na madini tukajua anatoka kwenye mgodi fulani tunarudi kwenye mgodi na kuchukua hatua tutafuta leseni hata kama umewekeza mabilioni.

“Tunazo taarifa wako wamiliki wengine wanatafuta watu wanawaambia pitisha ukitoka tutagawana riziki,mtagawana riziki ya kukosa leseni nimekuja kuwapa huo ujumbe na ukiona mfanyakazi wako amekamatwa huko ulipo beba leseni yako turudishie mwenyewe,” amesema Biteko na kuongeza kuwa;

“Broker au dealer  tukikutamata unatorosha madini au umetumia deiwaka wako tunamchukua na madini tunamuweka mahali na tunakufutia leseni na kutoza faini Sh Milioni 50 iliyopo kwenye sheria ili tuondoe wizi,”.

UKAGUZI GETINI

Kuhusu malalamiko ya kuchelewa kukaguliwa getini pamoja na kutokuwa na faragha kutokana na vyumba kuwa vichache, Biteko amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila kuwasiliana na Suma JKT ili ujenzi uanze mara moja.

“Mimi na naibu waziri hatuna mabegi ya kubeba kero tumekuja kutatua kero,ni kweli mbunge wenu ameeleza kwa uchungu.Ukuta utakuja na changamoto zake tulijua tutakagua hapa kumbe ni wengi hili lazima lifanyiwe kazi.

“Tutajenga jengo lengine na tutaweka paa ili kukiwa na mvua isiwanyeeshee au jua lisiwe kali,litasaidia kupunguza foleni ya ukaguzi,” amesema Biteko.

Kuhusu malalmiko ya baruti eneo moja,Waziri huyo amepiga marufuku kuendelea urasimu wa kibali cha kununua baruti eneo moja na badala yake kibali hicho ana uhuru ana kununua vifaa vya uchimbaji ikiwemo baruti katika eneo analotaka mwenyewe.

“Kibali cha baruti na unalazimishwa kwenda kununua sehemu moja,kuanzia leo ni marufuku kuĺazimisha mtu akanunue kama hapa una kibali cha kwenda kwa fulani kununua baruti mrudishie.

“Uwepo  wa ukuta utufikirishe wote ni kwa sababu kuna historia,tudhibitiane kwani mlolongo wa kodi za maudhi zikafutwa na masoko ya madini yakajengwa ila kama ilivyo kawaida wanadamu wamerudi misri,utoroshaji umerudi Mirerani,”amesema Biteko.

NAIBU WAZIRI

Nae, Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema uwepo wao hapo ni kujali na kuendelea kuonyesha serikali inatatua matatizo yanayokumba wananchi wake kwa kuongea pamoja ili waweze kufanikisha kutatua matatizo.

Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya.

“Kuhusu barabara ya ndani limeshafika ngazi ya Wizara na tumeshazungumza na Tarura na muda mfupi watazungusha barabara ya ndani ili kuwasaidia na kulinda miundombinu ikiwemo ya kamera.

“Laiti mngekuwa waaminifu na kutambua dhamira ya serikali kutaka Tanzanite iwe nembo ya kutambulisha Tanzania,tungetamani mtambue utoroshaji usiwe sehemu ya maisha yenu kwani katika kipindi cha miezi mitatu kuna matukio saba ya watu waliokamatwa wakitorosha madini,” amesema Prof. Manya.

MBUNGE

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ameiomba wizara hiyo kuangalia namba ya kuboresha faragha wakati wa ukaguzi kutoka katika eneo hilo la machimbo.

Amesema ukuta umejengwa ili kudhibiti madini lakini  kuna mambo hayajakamilika wanaingia kwa urahisi wachimbaji migodini lakini kutoka nje ya ukuta ni shughuli pevu.

“Wachimbaji na wamiliki wa migodi wanaingia kwa urahisi migodini lakini kutoka nje ya ukuta  ni shughulì pevu na ngumu ninahitaji nilete ombi kwani kabla ya kufika kwenye geti tunapita foleni kwa muda mrefu kama kuna mvua itakuwa halali yako hata kama ni masaa mangapi.

Christopher Ole Sendeka

“Tunaomba tupate paa liwekwe wakati tunatoka kabla ya kukaguliwa. Aidha vyumba vingozwe ili watu wawahi na kutaongeza faragha kwani huwez kumkagua mama wa miaka 65 na binti wa miaka 20 katika chumba kimoja na suala la faragha ni muhimu,” amesema Ole Sendeka.

Amesema kuwa katika mambo ya kiusalama taratibu lazima ziendelee kufuatwa lakini pia hiyo isiwe sababu ya wachimbaji hao kuvunja sheria ikiwemo wizi wa madini au udanganyifu kwani ni makosa ya jinai.

MAREMA

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa madini mkoa wa Manyara (Marema), Justine Nyari aliomba serikali kuangalia namna ya kuweka mazingira rafiki ikiwemo kibali cha kununua vifaa vya uchimbaji ikiwemo baruti.

Amesema kibali kimekuwa kikitolewa kwa masharti ya kununua baruti katika kampuni moja na iwapo utakosa utalazimika kulipia kibali tena ili ukachukue katika kampuni nyingine na kuomba kibali kitolewe na kiweze kutumika katika kampuni yoyote.

Mkuu wa Wilaya

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula amewataka wachimbaji hao kuhamasishana  kuacha utoroshaji wa madini kwani kadhia wanayokutana nayo inasababishwa na wachache wasio waadilifu.

“Ukitaka uheshimiwe lazima ujiheshimu,msingekuwa na tabia ya kudokoa au kutorosha madini pale getini hata askari tusingeweka.Jambo hili linasababishwa na wachache,ukaguzi utaendelea ingawa utaendelea kuboreshwa,”amesema Chaula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles