Ramadhani Hassan -Dodoma
SERIKALI imesema inaendelea kuratibu zoezi la upatikanaji wa bima ya afya kwa wote ili kila Mtanzania aweze kupata huduma za afya.
Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Edward Mmbanga, wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na Mifuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2012 unaonesha kaya ambayo zinaishi chini ya mstari wa umasikini zimepungia kutoka asilimia 28 hadi asilimia 26.
“Haiwezekani Serikali ikaacha kundi hilo kubwa, kwahiyo kinachofanyika sasa ni majadiliano ya kuona ni namna gani watu wasiokuwa na uwezo hawa asilimia 26 Serikali itawasaidia.
“Hivyo utakafika muda hawa nao waangaliwe. Sasa ndio maana ninaamini suala hili la bima ya afya kwa wote mtakuwa mnalisikia na kwanini Serikali haifikii mwisho.
“Serikali yoyote makini haikurupuki suala hili lipo katika mazungumzo na tutalikamilisha hivi karibuni. Wote mnajua nchi ilivyopata uhuru huduma karibia zote zilikuwa zinagharamiwa na Serikali kadri siku zilivyozidi kwenda iliweka utaratibu wa uchangiaji huduma hatua kwa hatua,”alisema.
Alisema kwenye sera ya afya ni kwamba watu maskini ni lazima wapate huduma bure ila kuna utaratibu.
“Kwahiyo nieleweke kwamba Serikali ipo katika hatua nzuri kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya. Hata wale wasiokuwa na uwezo utaratibu unawekwa vizuri,”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, alisema mkutano huo ni watano kukutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ambapo mwaka 2019 walikutana jijini Dar es laam na kushauriwa mambo mbalimbali ambayo NHIF wameishayatekeleza.
Aliyataja mambo waliyoshauriwa ni pamoja na kufanya maboresho ya huduma za afya, kuwafikia Watanzania wengi na kuviangalia upya vifurushi mbalimbali.
“Yale tuliyoshauriwa kwa kiasi kikubwa tumeyaweka vizuri, tulishauriwa suala la elimu na kiukweli tumewafikia Watanzania wengi kwa kuwapa elimu. Lakini pia tunapenda kufanya utafiti na waandishi wa habari, zile tafiti za kihabari,”alisema.
Konga alisema Serikali ilianzisha Mfuko wa Bima ya Afya mwaka 2001 kwa kusudi la kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.
Alisema katika Watanzania milioni 60 ni milioni 4.4 ndio wanatumia bima ya afya.