Na Sheila Katikula, Mwanza
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji amesema Serikali imetenga Sh bilioni 45 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa anwani za makazi na Postikodi katika Halmshauri 194 zilizopo nchini.
Dk. Kijaji amesema hayo juzi jijini Mwanza katika ziara ya Kamati ya Watalaamu wa Anwani za makazi iliyolenga kuona utekelezaji wa zoezi la anwani za makazi kama sehemu ya kujifunza kwa halmashauri zingine nchini.
Amesema lengo ni kuhakikisha kila mtaa unakuwa na jina lake na kila nyumba iwe na namba yake, ili kurahisisha utendaji kazi wa serikali katika shughuli za kiuchumi hususan uchumi wa kidijitali.
“Uchumi wa kidijitali hauwezekani bila kukamilisha mfumo huu wa anwani za makazi, tunamshukuru, Rais Samia Suluhu kutupatia fedha hizo ndani ya Wizara yangu kwa zoezi hili tu, kwa hiyo tunakwenda kukamilisha kwenye halmashauri zetu zote.
“Dhamira ya serikali ni kuwafikia wananchi kule walipo, kwani kutasaidia pindi anapopata tatizo, iwe rahisi kupata huduma ya zimamoto pindi watakapopata majanga ya moto au mgonjwa ukiwa unahitaji huduma ya gari ya wagonjwa,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema atahakikisha zoezi hilo linakamilika kwenye halmashauri zote mkoani hapa kama ilivyokuwa kwenye halmashauri ya Nyamagana.
Mwenyekiti wa kamati ya Wataalam wa anwani za makazi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mosses Seleki amesemajiji la Mwanza wamefanikiwa kufunga namba za anwani za makazi kwenye nyumba 108,000 na kuweka nguzo za mitaa 5,800.
Diwani wa Kata ya Nyamagana, Biko Kotecha ameipongeza Serikali kwa mpango wa anwani za makazi kwa kuwa mradi utarahisisha zoezi la utoaji huduma muhimu kwa wananchi wote.