Veronica Simba na Hafsa Omar, Dodoma
Serikali imetenga kiasi cha takribani Sh bilioni 18.6 kwa ajili ya kuvifikishia umeme vijiji vyote 42 vilivyopo wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma, ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani wakati akizindua Mradi Kabambe wa kusambaza umeme vijijini, Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili Ngazi ya Mkoa, uliofanyika Julai Mosi mwaka huu katika Kijiji cha Itaswi, wilayani Kondoa.
“Kijiji cha Itaswi ni moja kati ya vijiji 42 vilivyopo katika Wilaya ya Kondoa ambavyo hadi sasa bado havijafikiwa na huduma ya umeme. Hivyo basi, Serikali kwa kutambua hilo imetenga kiasi hicho cha fedha ili kukamilisha kazi hiyo,” alieleza Waziri.
Aidha, katika hafla hiyo, Dk. Kalemani aliwatambulisha Wakandarasi watakaotekeleza Mradi husika wilayani humo, ambao ni kutoka Kampuni ya Ok Electrical and Electronics Service Ltd na kuwataka wananchi ambao hawajafikiwa na umeme kutokuwa na shaka kwani Serikali imejipanga vema kuhakikisha wote wanafikiwa na nishati hiyo.
“Mkoa wa Dodoma kwa ujumla wake una vijiji 387 vyenye umeme kati ya 565 vilivyopo. Leo ninawakabidhi wakandarasi hawa kwenu wananchi ili kwa pamoja waushambulie Mkoa huu na kuhakikisha vijiji vyote 178 vilivyosalia vinapatiwa umeme,” alisisitiza.
Waziri aliwahamasisha wananchi kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili Mkandarasi atakapofika katika maeneo yao, wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.
Aliwashauri wananchi wenye nyumba ambazo siyo kubwa, kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (Rural Energy Board – REB), Wakili Julius Kalolo, alieleza kuwa malengo ya Serikali ni kusambaza nishati ya umeme katika vijiji vyote ifikapo Disemba 2022 na vitongoji vyote mwaka 2025.
Wakili Kalolo alieleza zaidi kuwa, utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, utaongeza uwekezaji wa miradi katika sekta mbalimbali vijijini ikiwa ni pamoja na kuanzishwa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.
“Aidha, miradi hii itaongeza ufanisi katika sekta ya madini kwa kufikisha umeme katika migodi ya wachimbaji wa madini hususani wachimbaji wadogo na wa kati,” alieleza Mwenyekiti.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga alieleza kuwa kuanzishwa kwa Wakala huo na utashi wa dhati wa Serikali, kumeleta mageuzi makubwa ya Sekta ya Nishati Vijijini ambapo upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka vijiji 518 sawa na asilimia 4 ya vijiji 12,268 mwaka 2007 hadi kufikia vijiji 10,312 sawa na asilimia 84 mwezi Machi, 2021.
Mhandisi Maganga alibainisha kuwa mafanikio hayo yamepatikana kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) kuanzia mwaka 2008, ambapo kiasi cha zaidi ya Sh trilioni 3.5 zimewekezwa. Uwekezaji huo umewezesha utekelezaji wa miradi kufikia hatua ya vitongoji.
“Hadi sasa, umeme umefika katika Wilaya zote. Aidha, Kata 3,225 kati ya 3,956 sawa na asilimia 82 na Vitongoji 26,860 kati ya 64,384,” alibainisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi wilayani humo akiwemo Mkuu wa Wilaya, Hamis Mkananchi na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dkt. Ashatu Kijaji walipongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali katika kupeleka umeme vijijini, hususani katika Wilaya hiyo.
Hata hivyo, viongozi hao waliomba kazi ya kukamilisha upelekaji umeme katika vijiji vilivyosalia, itekelezwe kwa kasi ili kukidhi kiu ya wananchi ambao wamejiandaa kupokea nishati hiyo ili waitumie katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo hivyo kuboresha maisha yao.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali, Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini Mhandisi Francis Songela, Louis Accaro, Oswald Urasa na viongozi wengine mbalimbali pamoja na wananchi.