22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi apiga marufuku Wakurugenzi kuchukua ardhi ya mtu kisa hajalipia

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema ni marufuku kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji mbalimbali kuchukua ardhi ya mtu kama hawana fedha ya kulipa fidia.

Pia amesema hivi karibuni Serikali itasajili madalali wote lengo likiwa ni kuondoa utapeli ambao umeendelea kuwepo kwa baadhi ya madalali ambao sio waaminifu.

Akizungumza leo Ijumaa Julai 2,2021 na Watendaji wa Ardhi mkoani Dodoma, Waziri Lukuvi amepiga marufuku kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na watendaji mbalimbali nchini kuchukua ardhi ya mtu kama hakuna fedha ya kulipa fidia.

Kikao hicho kiliandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kwa ajili ya kusaidia kutatua migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma.

“Kiongozi wa serikali hawezi kuwa mwizi, Dodoma mlikuwa mnatumia ubabe sana, ardhi ni yangu lazima tuelewane, kwenye ardhi hakuna ubabe lazima tusimamie sheria. Usiitamani ardhi ya mtu tafuta hela Mkurugenzi kama huna hela ya kulipa achana nae.

“Hatuwezi kuendeleza migogoro unataka kujenga Zahanati kwenye ardhi ya mtu lipa kwanza fidia ndio uendelee na ujenzi hata kwenye dini wanasema usitamani kisichochako, huna hela niachie ardhi yangu lakini fidia lazima unipe,”amesema.

Amesema kwa sasa serikali itasajili madalali wote ili kuondoa utapeli ambao umekuwa ukitokea katika ardhi.

“Kamateni matapeli kwa Dodoma ni wengi na wanaendelea kuwaibia watu. Sasa tunakuja na mfumo wa kusajili madalali wote na lazima awe na ABC katika ardhi kwani wengi ni wezi tu,”amesema.

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka ametangaza kuanzia Jumatatu ya Julai 5, mwaka huu timu ya wataalamu wa ardhi kutoka Jiji la Dodoma itakuwa kwa siku tatu katika ukumbi wa JK mkoani hapa ikipokea kero mbalimbali zinazohusu migogoro ya ardhi.

Mtaka amesema mara baada ya kusikiliza kero hizo kwa siku tatu watatembelea kata 41 kwa ajili ya kutatua migogoro hiyo kwa vitendo.

“Tunawakaribisha wale wote wenye matatizo ya ardhi kuanzia Jumatatu timu yetu ya wataalamu itakuwepo kwa ajili ya kutatua matatizo ya ardhi katika Jiji la Dodoma.Mashauri yote yatasikilizwa kama ni familia waje wote na nyaraka ili iwe rahisi kwa wataalamu wetu kuitatua,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles