MIONGONI mwa makosa ambayo Marais wengi wa Afrika wanayafanya ni kudhani kuwa kuviangamiza vyama vya upinzani ndio mwarobaini wa kuleta maendeleo.
Fikra za namna hii zinasababisha kuviona vyama vya upinzani kama uasi ni mfu kwani maendeleo kamwe hayawezi kupatikana kwa mtazamo na akili ya mtu mmoja pasipo nguvu ya mawazo kinzani kutoka kwa wengine.
Inasikitisha sana kwamba pamoja na mataifa mengi ya Afrika kuukubali mfumo wa vyama vingi katika miaka ya 1990 na kuendelea bado kuna hali ya sintofahamu kwani kila kukicha ni vurugu zitokanazo na mnyukano wa kisiasa.
Ni kweli wengine wanaweza kusema nchi nyingi za Afrika ziliukubali mfumo wa vyama vingi kutokana na shinikizo la mataifa magharibi na wala haukuwa utashi wao kwani watawaliwa wengi wakiwamo wa Tanzania bado walitamani kuendelea na mfumo wa chama kimoja lakini la kujiuliza ni nini kilisababisha wapigania uhuru wa awali kama Mwalimu Nyerere kuuridhia mfumo huu?
Je, hayati Mwalimu Nyerere ambaye wengi wetu tunamhusudu kwa mazuri aliyoyafanya, kuubali mfumo wa vyama vingi ilikuwa ni usaliti ukizingatia alikuwa ameishastaafu au ni jicho pevu alilokuwa nalo kwa kuona yatakayotokea mbele maana alianza kushuhudia viongozi wakigeuka miungu watu badala ya kuwatumikia wananchi?
Ni ukweli usiopingika Mwalimu Nyerere alizisoma alama za nyakati na kutambua kuwa chama tawala bila kupata nguvu ya kukosolewa kinaweza kujisahau na hatimaye siku moja kuitumbukiza nchi kwenye shimo refu la migogoro pale wananchi watakapoanza kuhisi kunyanyaswa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Si tu ni Mwanamapinduzi Nyerere aliyependelea mfumo mpya wa vyama vingi bali pia hata tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mfumo huu unayo nguvu ya kuifanya serikali iwajibike na hatimaye kuleta maendeleo tarajiwa.
Kwa mujibu wa (Mililler 2000) anasema demokrasia ya vyama vingi, vyama vya siasa huwajibika na pia kuwa kiungo muhimu kati ya serikali iliyoko madarakani na raia ambao kimsingi maslahi yao hupata nguvu ya utetezi kwa kuchochea sera na watunga sera ili waweze kufikia maamuzi sahihi.
Si tu kutetea nguvu ya sera na watunga sera pekee bali pia vyama vya upinzani vinao uwezo wa kuisimamia serikali ili iwatumikie raia wake ( Burnell 2004)
Wakati umewadia kwa viongozi wakuu wa nchi hususani wa Bara la Afrika kuukubali na kuuchochea mfumo wa vyama vingi kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo na kuepuka migogoro isiyo na sababu za msingi.
Ni ulevi wa madaraka ni ufinyu wa fikra kwa kiongozi yeyote kusimama hadharani na kutamka kuwa nchi inakosa maendeleo kutokana na uwepo wa vyama vingi.
Ni kweli kuna ushahidi finyu wa kitaaluma unaoonesha uhusiano kati ya demokrasia ya vyama vingi na maendeleo kwani China mbali na kubinya demokrasia bado maendeleo yake yanakuja kwa kasi lakini Je, vipi kwa mataifa ya magharibi yenye maendeleo ya muda mrefu tena ndani ya vyama vingi?
Kama vyama tawala vinawajibika ipasavyo kwa wananchi huku maendeleo yakionekana waziwazi, hofu ya kuogopa ukosoaji wa vyama vya upinzani inatoka wapi?
Wapigania uhuru wetu mfano Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hawana budi kuenziwa na viongozi wa Afrika hasa walioko madarakani kwa kuwekeza kwenye Katiba imara zitakazoimarisha mifumo ya vyama vingi vya siasa, kuheshimu mihimili mingine ya mahakama na Bunge bila kusahau taasisi za kiraia na vyombo vya habari.