JUMA lililopita tulikumbushana mambo mbalimbali yanayohusu umuhimu wa kula mlo kamili ili kuujenga mwili kiafya.
Pia tuliona ni kwa namna gani mjamzito anaweza kupata matatizo ya meno kutokana na kupungukiwa madini ya ‘calcium’ mwilini.
Nichukue fursa hii kukufahamisha miongoni mwa kazi na umuhimu wa madini mbalimbali mwilini.
Tukumbuke kwamba, tunaposema madini au kwa kitaalamu elements tunamaanisha vitu ambavyo kimsingi husaidia mwili katika kufanya kazi zake kwa kadiri inavyopaswa.
Vitu hivi huingia mwilini kupitia vyakula na vinywaji mbalimbali ambavyo tumekuwa tukivitumia kila siku.
Miongoni mwa madini hayo ni pamoja na kalsium, potassium, chloride, zinc na sodium. Yapo madini mengi yenye umuhimu mwilini, lakini pengine nikupitishe katika hayo machache.
Kalsium ni madini ambayo umuhimu wake mwilini ni katika kuimarisha mifupa na meno. Aidha, madini haya yamekuwa yakisaidia ufanyaji kazi wa misuli ya mwili/moyo.
Hali ya moyo kuweza kusinyaa na kutanuka (heart contraction) na kusukuma damu mwilini, inawezeshwa na madini haya. Hivyo, ufanyaji kazi wa moyo umekuwa ukisaidiwa na uwapo wa madini haya mwilini.
Katika ufanyaji kazi wa moyo, pia sambamba na madini ya kalsium, yapo madini mengie ya potassium ambayo husaidia kuhakikisha moyo na mwili kwa ujumla vinafanya kazi katika hali inayotakiwa. Usafirishaji wa taarifa kupitia mishipa ya fahamu na mawasiliano katika seli mwilini huhitaji uwapo wa madini haya.
Pia katika kuwezesha mawasiliano mazuri baina ya mishipa ya fahamu mwilini, kuna ufanyaji kazi wa pamoja baina ya madini ya sodium pamoja na potassium (Na/K Pump). Kwa pamoja madini haya huzifanya seli za mwili kuwa katika njia nzuri ya kuwasiliana (Action Potential) na kutuma taarifa katika maeneo mengine ya mwili.
Aidha, katika figo madini ya sodium husaidia mwili kukusanya maji na kuyazuia yasitoke kupitia njia ya mkojo. Uwapo wa sodium nyingi katika mwili husababisha maji mengi kuhifadhiwa mwilini. Hii husababisha ujazo wa damu kuongezeka na hivyo kusababisha mtu kuwa katika hatari ya kupata shinikizo la juu la damu. Hii imekuwa sababu ya watu kushauriwa kutotumia chumvi nyingi katika vyakula ili kuepuka hatari hii ya maji mengi kuhifadhiwa mwilini na hatimaye presha kupanda.
Kwa madini ya chlorine(chloride), haya hushirikiana na madini mengine mwilini mfano, potassium na sodium katika kuhakikisha ujazo wa damu unakuwa imara. Lakini pia kurekebisha hali ya tindikali au base mwilini, (Acid – Base balance). Madini haya ni sehemu muhimu ya acid aina ya HCL iliyopo tumboni ambayo husaidia kufanya mmeng’enyo wa vyakula hususani jamii ya protini.
Madini jamii ya zinc, husaidia kuifanya kinga ya mwili ifanye kazi vizuri, kukua na kugawanyika kwa seli mwilini na kuwezesha majeraha kupona kwa haraka.
Katika matumizi ya kawaida ambayo pengine utaweza kukumbuka ni kwamba mara zote watoto wadogo wanapopatwa na tatizo la kuharisha, wakifika katika vituo vya tiba huwa wanapatiwa dawa ya kuchanganya na maji na kunywa (ORS) na vidonge vya zinc.
ORS huwasaidia wagonjwa wanaoharisha au kutapika kurejesha madini yaliyopotea, pia dawa ya zinc husaidia kupunguza namna ambavyo utumbo unajikunja na hivyo kumsaidia mgonjwa kupunguza kuhara (reducing frequency or motion).
Madini haya yanapokosekana au kupugua mwilini, husababisha mwili na mifumo mingine ishindwe kufanya kazi vizuri. Kukosekana kwake kunaweza kuifanya mishipa ya fahamu ishindwe kufanya kazi vizuri, moyo kushindwa kufanya kazi na kumfanya mtu apate dalili mbalimbali ikiwamo kwikwi.
Katika vituo vya tiba hali hii imekuwa ikitibiwa kwa njia ‘drip’ ili kumwezesha kurejesha madini yaliyopotea na kuiimarisha afya ya mgonjwa.