NAIROBI, KENYA
CHAMA cha Wiper Movement kimeweka msimamo wa kutaka kiongozi wake, Kalonzo Musyoka atangazwe kuwa mgombea urais wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa), vinginevyo kijitoe.
Kiongozi wa Walio Wachache Bungeni ambaye ni mshirika wa Musyoka, Francis Nyenze alionya utakuwa mwisho wa NASA iwapo kiongozi wa Wiper atanyimwa tiketi ya kuuwakilisha umoja huo katika uchaguzi wa Agosti 8 mwaka huu.
“Hili ni onyo la mwisho, iwapo Kalonzo hatakuwa mgombea urais, Nasa kamwe haitakuwepo,” aliuambia mkutano wa waandishi wa habari katika majengo ya Bunge mjini hapa jana.
Chama hicho kinataka kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga aheshimu hati ya makubaliano (MoU) aliyosaini na Musyoka mwaka 2013.
Viongozi wa Wiper wamekuwa wakidai vinara hao wenza wa NASA walikubaliana Odinga awe mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2013 na Musyoka agombee mwaka 2017.
Nyenze alisema ameipa Nasa siku saba kuitisha mkutano wa Kamati ya Taifa ya uratibu kupitia makubaliano ya 2013, vinginevyo Musyoka atajitoa.
"Jamii ya Wakamba imefikia uamuzi kuwa iwapo si Kalonzo, Wiper itaenda peke yake," alisema.
Saa chache baadaye jana, Katibu Mkuu wa Wiper, Hassan Omar alihutubia mkutano ambao ulikuwa uhudhuriwe na Musyoka.
Hata hivyo, Musyoka aliondoka dakika chache baadaye, akisema amepata kikao muhimu cha dharura.
Omar alithibitisha kauli iliyotolewa na Nyenze lakini aliongeza kuwa Wiper itashiriki ndani ya Nasa hata kama Kalonzo hatateuliwa kupeperusha bendera ya muungano huo.
Omar alishutumu mkwamo uliopo ndani ya Kamati ya Taifa ya Uratibu, iliyopewa jukumu la kuandaa namna ya kumchagua mgombea urais wa muungano huo.
Mpango huo umeshindikana tangu Desemba mwaka jana na kuzua hofu juu ya hatima ya muungano huo uliopania kukiondoa madarakani chama cha Jubilee.