WASHINGTON, MAREKANI
Joe Biden amepata ushindi mkubwa katika kura ya uteuzi wa mgombea wa chama cha Democratic jimboni South Carolina akipata kuungwa mkono na Wamarekani weusi na kufikisha mwisho ushindi mfululizo wa Bernie Sanders.
Ushindi wa Biden umekuja katika wakati wa kufa na kupona katika mwaka 2020 wakati mwanachama huyo wa chama cha Democratic mfuasi wa siasa za wastani akirejea katika mbio hizo baada ya kushindwa katika majimbo ya Iowa, New Hampshire na Nevada.
Mbio hivi sasa zinaingia katika awamu mpya wakati majimbo 14 yatakapoanza rasmi kampeni katika kile kinachofahamika kama Jumanne Kuu.
“Bado tuko hai. Kwa nyie wote ambao mmeanguka, jihesabuni mmeondolewa, mmeachwa nyuma , hii ndio kampeni yako,” Biden alisema katika mkutano wa baada ya uchaguzi.
Sanders amepata nafasi ya pili, licha ya kuwa kushindwa kwake kumetoa ahueni ya muda kwa wademokrat wenye shauku ambao wanahofia kuwa mwanasiasa huyo aliyejitangaza kuwa ni msoshalist ataibuka mwezi Februari kwa ushindi wa majimbo manne.
Mwanaharakati tajiri, bilionea Tom Steyer , ambaye alikuwa akipambana ili kupata nafasi ya tatu, amesitisha rasmi kampeni yake.
Alitumia zaidi ya dola milioni 19 katika matangazo ya televisheni katika jimbo la South Carolina, fedha nyingi zaidi kuliko wapinzani wake wote kwa jumla, lakini hakuweza kupata njia katika mpambano huo wenye wagombea wengi.
Wagombea saba wanaendelea na mbio zao kutaka kuteuliwa na chama cha Democratic kupambana na rais wa sasa Donald Trump mwezi Novemba.
Washirika wa Biden haraka waliuelezea ushindi huo wa South Carolina kuwa ushahidi kuwa anapaswa kuwa mgombea wa chama hicho akiwa ni mbadala wa wazi wa Sanders.
Uchaguzi wa mchujo katika jimbo la South Carolina ni mtihani wa kwanza mkubwa kwa wagombea miongoni mwa wapiga kura weusi.
Na kwa kuwa umempa Biden mwenye umri wa miaka 77 ushindi ambao alikuwa akiuhitaji mno, ni lazima athibitishe kuwa ana vitendea kazi pamoja na uwezo wa kifedha kupanua kampeni yake katika muda wa masaa 72 yajayo.
Pia atakuwa katika shinikizo kutegemea uhusiano wake wa muongo mmoja na viongozi wa chama kutengeneza hali mpya ya kwamba inawezekana katika kugombea kwake.
Shirika la habari la Associated Press lilitangaza Joe Biden mshindi , muda mfupi tu baada ya upigaji kura katika jimbo la South Carolina.