RAIS wa Marekani Joe Biden amesema nchi yake itajitolea kuitetea Taiwan endapo China itaishambulia hatua ambayo inapingana na sera ya muda mrefu ya Marekani ya ‘Utata wa Kimkakati’.
Kwa mujibu wa CNN, Biden amesema hayo jana alipoulizwa kuwa Marekani ipo tayari kuilinda Taiwan na kusema “Ndio, tuna dhamira ya kufanya hivyo,”.
Hata hivyo baadaye msemaji wa Ikulu aliviambia baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani kwamba matamshi hayo hayakuashiria mabadiliko ya sera.
Marekani haina uhusiano wowote wa kidiplomasia na Taiwan, lakini inauza silaha kwa kisiwa hicho kama sehemu ya Sheria ya Uhusiano ya Taiwan, ambayo inasema kuwa Amerika lazima isaidie Taiwan kujilinda.
Mvutano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiongezeka katika wiki za hivi karibuni baada ya Beijing kurusha ndege kadhaa za kivita katika eneo la ulinzi wa anga la Taiwan.