BERLIN, UJERUMANI
MAELFU ya watu wenye kutia shaka kuhusu janga la virusi vya corona nchini Ujerumani wameanza kukusanyika mjini Berlin katika maandamano makubwa ya kupinga vizuizi vilivyowekwa na serikali.
Maandamano hayo yameruhusiwa kufanyika baada ya mapambano makali mahakamani.
Polisi imesema itaweka ulinzi na kufuatilia kanuni ya uvaaji barakoa na watu kutosogeleana.
Mkuu wa polisi Berlin, Barbara Slowik ameonya kuwa kama waandamanaji hawatazingatia kanuni za usalama kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, polisi watayavunja maandamano hayo haraka sana.
Maofisa wa mji wa Berlin awali waliamua kutoyaruhusu maandamano hayo ya leo, wakihofia kuwa idadi inayokadiriwa ya waandamanaji 22,000 hawatazingatia masharti ya kukaa umbali wa mita moja na nusu au kuvaa barakoa.
Lakini katika mkesha wa maandamano hayo, mahakama ya Berlin iliwaunga mkono waandamanaji, ikisema hakuna dalili kuwa waandalizi watapuuza makusudi kanuni hizo na kuhatarisha afya ya umma.
Wakati huo huo,
Maelfu ya waandamanaji wanaodai kukomeshwa kwa ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi wamemiminika katika mji mkuu wa Marekani, Washington, kuashiria hasira iliyoibuka upya na kulikumba taifa hilo baada ya tukio jingine la kupigwa risasi Mmarekani mweusi Jacob Blake na polisi mzungu.
Umati mkubwa wa watu ulikusanyika katika eneo la makumbusho la Lincoln Memorial katika kumbukumbu ya miaka 57 tangu hotuba maarufu ya “I have a dream” yaani “nna ndoto” iliyofanywa mahala hapo na mwanaharakati wa haki za kiraia Martin Luther King Jr. Agosti 28. 1963.
Maandamano hayo yaliandaliwa baada ya kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd katika tukio la kikatili lililofanywa na polisi mjini Minneapolis mwishoni mwa mwezi Mei.