25.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Jafo awasisitiza viongozi wa dini kuombea nchi

Ramadhan Hassan-Dodoma

KUELEKEA uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani katika nyumba za ibada.

Kauli hiyo aliitoa jiji Dodoma jana, wakati akifungua  semina elekezi kwa viongozi wa dini kuhusu amani kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.

Semina hiyo iliandaliwa Taasisi ya  Markaz Islaam ya Chang’ombe ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dodoma.

Waziri Jafo alisema amani ni muhimu kipindi hiki nchi ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu.

“Twendeni tukahubiri amani hakuna binadamu ambaye aliyekamilika ila lazima tuvumiliane,tupime nia za watu,tuna kila sababu ya kuendelea kupendana.

“Viongozi wa kisiasa nao wanawajibu wa kuendelea kuhubiri amani.Mataifa yote yanayotuzunguka yote yamepata misukosuko ukienda hapo Kongwa unaona kambi tulikuwa tunawalea,sisi Tanzania tunawajibu wa kuendelea kulinda amani.

“Bahati mbaya kila mtu ana urefu wa kamba yake amani ikiharibika kesho hayupo..mwenzangu na mimi imejitahidi  umeenda Chemba, mwingine kakimbilia Kondoa,mwenzako ana pasipoti  mbili mambo yakiharibika tu huyoo,”alisema Jafo.

Aliwaomba maimamu wa misikiti wawe wanaweka kipengele cha kuhubiri amani kwa waumini wao, wakati wa ibada ya swala ya Ijumaa.

“Agenda ya amani ni msingi wa kila kitu tuna siku kadhaa za kwenda katika uchaguzi mkuu,fursa hii inatakiwa pia kuwepo  katika hotuba za maimamu tuwe tunaweka kipendele cha amani.

“Amani inapopotea watu wenye vyeo vyao wanakuwa madhalili,matajiri wanakuwa masikini mfano Libya ya zamani na sasa tuangalie ilivyo sasa, mabwana wamegeuka kuwa watwana.

“Amani ndio jambo kubwa katika maisha ya binadamu,wenzetu wanaishi kwa kujificha wengine wanafanya ibada silaha ipo pembeni tena inawezekana wa imani moja.Hakuna jambo linalouma kama familia,kudhalilishwa kama binadamu.

“Bila amani mke wako atadhalilishwa mbele yako,amani ndio jambo kubwa sana katika maisha ya binadamu angalia ndugu zetu wa Yemeni, Syria,Jamhuri ya Afrika ya Kati kila mtu analala kwenye nyumba yake hajui kama kesho ataaamka,”alisema.

Alisema amani ikipotea uchumi wa Nchi utayumba hivyo kila mmoja anawajibu wa kuilinda.

“Bahati mbaya maadui wanaingiza mambo yao wakati wa uchaguzi kipindi hichi viongozi wa dini mnapaswa kusimamia amani, mnapaswa kuzifanya roho za binadamu ziwe na utu.

“Amani ikiondoka hakuna kufanya kazi,amani inaenda sambamba na uchumi kama kuna watu wana nia mbaya kuja kuharibu uchumi.

Aliwataka viongozi wa dini mikoa mingine kufanya semina elekezi kwa viongozi wa dini katika mikoa yao.

“Viongozi tuendelee kutoa maneno mazuri kwa vijana kwenu wengine wanalipuka tu,tujivunie tumetengeneza Taifa bora mara baada ya uchaguzi,”alisema Jafo.

Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu alisema  kazi za kijamii zinahitaji ushirikiano mkubwa na dini zote zinatakiwa kushirikiana.

“Jukumu la kulinda amani ni letu sote,mwenyezi Mungu hajawakata kushirikiana yapo mambo sisi kama waislamu tunaweza kushirikiana nayo na miongoni mwao ni ujamii ambayo hatuwezi kushirikiana ni masuala ya kiitikadi na kiibada.Unaweza kushirikiana katika ugonjwa,kukopeshana,kuishi pamoja.

Aliwataka masheikhe wa misikiti kuhubiri amani huku akitaka kutoruhusu nyumba za ibada kutumiwa na wanasiasa kufanya kampeni katika misikiti.

“Niwatake masheikhe kuhubiri amani,amani yetu furaha yetu,tusikubali msikiti wowote kuvunjwa amani,ukijinasibisha na kundi fulani la kisiasa wewe utakuwa chanzo cha uvunjifu wa amani,sisi la kwetu ni kuwaelekeza kudumisha amani na kuwagundua wahalifu.

“Kuna baadhi ya misikiti na makanisa wanatumia kama sehemu za kuhubiri siasa hapa kwetu haipo,hukatazwi kuwa muumini wa chama chochote waachie wanasisa,”alisema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Markaz Islaam Chang’ombe, Dar es Salaam,Dk.Kamal Abdul Mut’wi alisema lengo la semina hiyo ni kueneza amani pamoja na kuonesha mtazamo wa amani kwa waislamu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Binilith Mahenge alisema watu wengine kipindi cha uchaguzi huwa wanaingiza mambo yao hivyo ni jukumu la viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani.

“Naamini tutafanikiwa na tutavuka kipindi hiki.Tunaomba amani na tunaomba kura za rais wetu,”alisema. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,Gilles Muroto alisema,amani ni muhimu kila sehemu, alishukuru kwa semina hiyo kufanyika Dodoma.

“Niseme tu na mimi familia yangu ni ya kiislamu,ushirikiano huu tumeanza katika familia uislamu na ukristo unamtegemea na kumwabudu mungu mmoja,tutunze amani hakuna pa kwenda Nchi yetu ni hii,”alisema Muroto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles