24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Benki zakomaa kutoza VAT wateja wake

Dk. Charles Kimei
Dk. Charles Kimei

NA Christina Gauluhanga, Dar es Salaam

SIKU chache tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuzitaka benki zote nchini kuacha kuwataka wateja wao kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), benki zimeibuka na kusema kuwa wataendelea kukata tozo hizo.

Hatua hiyo inatokana na utekelezaji wa sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ulioanza Julai Mosi mwaka huu na kuzua mkanganyiko kwa wananchi baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mabenki kutofautiana jinsi ya ukusanyaji wake.

Kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge lililomaliza mkutano wake Juni 30, mwaka huu mjini Dodoma, taharuki na malalamiko yamekuwa yakitawala kila kona huku wananchi wanaotumia huduma za kibenki na miamala ya kifedha kwa njia ya simu wakiwa hawajui ni nani hasa atakayebeba mzigo wa kodi hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha wenye mabenki Tanzania katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Dk. Charles Kimei, alisema mabenki hayawezi kuepuka kuwatoza wateja wake kodi ya ongezeko la thamani VAT.

Alisema kutokana na sheria hiyo benki zote yameongeza kiasi kidogo cha makato ili kufidia VAT.

“Ukataji wa VAT kwa wateja wa mabenki haukwepeki japokuwa ni asilimia ndogo lakini mteja lazima achangie na ndiyo maana halisi ya VAT, mteja analipa kutokana na huduma anayoipata,”alisema Dk. Kimei ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.

Alisema pamoja na ufafanuzi wa Serikali ya kuzitaka benki zote kutomtwisha mteja makato hayo ambapo awali alikuwa akikatwa Sh 200  lakini baada ya sheria hiyo itaongezeka na kufikia Sh 236.

Alisema ongezeko hilo ni dogo ambalo limesababishwa na huduma waipatayo benki.

Pamoja na hali hiyo alisema benki zote hazitakwenda kinyume na sheria na watahakikisha asilimia 18 inalipwa kama sheria inavyotaka.

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa wamepewa jukumu la kukusanya kodi kwa wananchi hivyo watatekeleza agizo hilo.

Akizugumzia utendaji kazi wa Benki ya CRDB, alisema kuwa wamefanikiwa kuongeza idadi ya wateja wao wapya na kufikia 520 kupitia maonyesho ya Sabasavba huku wateja 600 wakijiunga na huduma ya Simu Banking.

Tangu Julai mosi mwaka huu, watumiaji wa huduma wa kibenki wanakatwa asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani kwenye kila muamala wanaoufanya ambayo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na TRA ni ongezeko la Sh 152.50 katika kila makato ya Sh 1,000 yanatozwa na benki mteja anapofanya muamala.

Kwa upande wa miamala ya fedha ya simu za mkononi za Vodacom, Tigo, Airtel na Ezy Pesa, mtu anayetuma Sh 10,000 atakatwa Sh 250 pamoja na asilimia 18 ya VAT jumla atakatwa Sh 1,250, jambo ambalo mamlaka za Serikali zimepiga marufuku.

Katikati ya sintofahamu hiyo ambayo msingi wake ni tamko lililotolewa na benki mbalimbali zinazofanya shughuli zake hapa nchini, likieleza kuwa kuanzia Julai Mosi, mwaka huu  ada na makato yote ya kibenki kwa wateja yatatozwa kodi ya ongezeko la thamani.

Mamlaka ya Mapato (TRA) imepiga marufuku mteja  kutozwa kodi hiyo, huku ikitishia kuchukua hatua kwa benki zitakazotekeleza makato hayo kwa wateja wake.

Kutokana na hali hiyo Julai 2, mwaka huu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata,  alitangaza kupiga marufuku kwa mabenki nchini kukata asilimia 18 ya VAT kwa mteja.

Alisema makato ya kodi ya VAT katika miamala ya fedha itakayofanywa na wananchi itatokana na ada za huduma ambayo mteja ametozwa na taasisi ya fedha inayompatia huduma.

Kamishna huyo wa TRA, alisema kuwa hakuna makato yatakayofanyika katika amana ya mwenye fedha na kwamba benki au taasisi yoyote ya fedha itakayoongeza makato kwa mteja wake kwa makusudi au kwa kisingizio cha kulipia kodi itachukuliwa hatua za kisheria.

Alifafanua kuwa Benki Kuu (BoT),  ina jukumu la kudhibiti benki zote nchini zisiwakate wateja wake asilimia 18 ya kodi ya VAT juu ya makato ya huduma zinazotozwa sasa na kwa upande wa kampuni za simu jukumu hilo ni la TCRA.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu Profesa Beno Ndulu, alinukuliwa na vyombo vya habari ambapo alisema VAT hutozwa kwa mtumiaji wa mwisho wa huduma za kibenki na kusisitiza kwamba siku zote mzigo wa VAT humwangukia mtu wa mwisho ambaye ni mteja wa benki.

Alisema taasisi za kibenki ni wakala wa Mamlaka ya Mapato (TRA) katika makusanyo ya kodi ya VAT hivyo kazi yake ni kukusanya kodi kwa niaba ya mamlaka hiyo kutoka kwa wateja wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles