22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya Afrika yataja maeneo ya kipaumbele Sadc

ANDREW MSECHU

BENKI Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetaja maeneo 10 muhimu inayosimamia katika kuhakikisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), zinakuwa na miundombinu wezeshi ya barabara na nishati, kama kichocheo cha kufikia malengo ya ukuaji wa uchumi

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha marais kwenye mkutano wa 39 wa SADC jana, Rais wa AfDB, Dk Akinwumi Adesina, alisema benki hiyo inaendelea kuthamini umuhimu wa SADC na katika ukanda wa nchi hizo, tayari imeshawekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 13.

Alisema benki hiyo haioni tatizo kuwekeza kiasi hicho kwakuwa uwekezaji huo unalipa na katika kila dola inayowekezwa kama mtaji, inarejesha dola 19 katika uwekezaji huo, ambayo ni uwiano mzuri wa 19:1.

Alisema maeneo waliyowekeza ni katika nishati, barabara, maji, bima ya biashara, uboreshaji wa mifumo ya kodi ya mapato na mikopo kwa nchi zenye uhitaji maalumu.

“Benki hii inaendelea kutambua umuhimu wa kipekee wa ukanda wa SADC, hasa wakati huu ambao tumekuwa tukiimarisha utendaji wa benki hii. Tayari, tangu nilipoingia mwaka 2015 tumeshafungua ofisi za kikanda katika kanda tano, ambazo ni za Magharibi, Mashariki, Kati, Kaskazini na Kusini mwa Afrika na tumeshafungua ofisi kwenye nchi 41,” alisema.

Alisema katika nishati tayari benki hiyo imeshawekeza dola bilioni tano kupitia kampuni ya ESKOM ya Afrika Kusini, inayounganisha nchi nyingi za SADC.

Alisema katika nishati pia, wamefanya juhudi za makusudi kusaidia uendelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme katika bwawa la INGA lililopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) lenye uwezo wa kutoa megawati 44,000 iwapo litarutubishwa ipasavyo.

“Tayari benki hii imeshatoa dola milioni 75 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika uzalishaji wa megawati 4,800 ambazo zitasaidia upatikanaji wa umeme kwa DRC, Afrika Kusini na maeneo mengine na tuko tayari kuwezesha uwekezaji utakaohitajika katika kutimiza adhma hii,” alisema.

Alisema katika uwekezaji mwingine, benki hiyo imeelekeza nguvu katika ujenzi wa barabara kwa kuhakikisha ndoto ya kuunganisha Cape Town Afrika Kusini hadi Cairo Misri inatimia.

Alisema kupitai kwa Rais John Magufuli, wameshatia saini ujenzi wa kilometa 251 kutoka Dodoma hadi Babati, ikiwa ni sehemu ya mpango huo wa barabara kuu itakayounganisha Afrika kutoka Cape town hadi Cairo kipitia Lusaka Zambia, ambayo kwa Tanzania itapita kwenye miji ya Dodoma, Arusha, kisha Nairobi Kenya.

Alisema katika hilo, AfDB pia inasaidia Serikali za visiwa vidogo ikiwemo Shelisheli na Comoro, kujenga miundombini ya barabara na ya maji.

“Lakini pia, benki hii imedhamini ujenzi wa Bandari ya Walvis Bay nchini Namibia kwa gharama ya dola milioni 300 za Marekani, ambayo itasaidia nchi za Zambia, Botsana na Zimbabwe na katika hili, ninampongeza Rais Hage Geingob kwa kuzindua upanuzi huo wiki chache zilizopita.

Alisema benki hiyo pia inadhamini ujenzi wa daraja la Kazungula litakaloziunganisha Zambia na Botswana na kurahisisha mawasiliano kwa Malawi na DRC, pia kuwezesha matumizi ya korido ya Nacala, kwa gharama ya dola milioni 500 kwa ajili ya ukanda wa SADC, ambapo uwekezaji huo utasaidia kuongeza biashara kikanda kwa asilimia 25 na kupunguza gharama za usafirishaji kwa asilimia 25.

Dk Adesina alisema benki hiyo pia imetoa dola milioni 300 kwa ajili ya kufadhili bima kwaajili ya biashara kwa Benki ya ABSA na Frist Rand za Afrika Kusini, ambayo itawezesha biashara zenye thamani ya dola bilioni mbili katika nchi 20.

“Benki pia imetoa dola milioni 25 kwa ajili ya kuwezesha Benki ya Maendeleo ya Eswatini na dola milioni 80 kwa Shirika la Maendeleo la Botswana kwa ajili ya kuwezesha wajasiriamali wadogo na wa kati,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles