MIAMI, MAREKANI
NYOTA wa zamani wa timu ya Manchester United, David Beckham, mwishoni mwa wiki iliopita alikutana na baba wa Lionel Messi kwa ajili ya kuzungumza juu ya uhamisho wa mtoto wake huyo mwishoni mwa msimu huu.
Beckham ni mmoja kati ya watu wanaomiliki timu ya Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani. Kwa mujibu wa gazeti la The Sun nchini Uingereza, uongozi wa timu hiyo ulifunga safari hadi jijini London kukutana na baba wa Messi, Jorge na kuona uwezekano wa kutaka kumsajili staa huyo wa Barcelona.
Baba wa Messi amekuwa akishughulikia mambo yote ya uwakala wa mchezaji huyo na kuna taarifa kwamba Messi anaweza kuondoka mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Wiki iliopita rais wa Barcelona, Josep Bartomeu, aliweka wazi kuwa Messi anaweza kuondoka ndani ya kikosi hicho kila ifikapo Juni 30 akiwa mchezaji huru kutokana na mkataba wake mpya mara baada ya kufikisha umri wa miaka 32.
“Messi amesaini mkataba hadi 2021, lakini tuna makubaliano naye kuwa anaweza kuondoka kila ifikapo Juni 30 akiwa mchezaji huru,” alisema rais huyo.
Kutokana na mkataba huo mpya wa Messi, klabu mbalimbali zimeanza kujiandaa kwa ajili ya kuwania saini ya mchezaji huyo mwishoni mwa msimu huu.