NYOTA wa zamani wa klabu ya Manchester United, David Beckham, amemtaka mshambuliaji mpya wa klabu hiyo, Memphis Depay, kuivaa jezi namba saba bila wasiwasi.
Beckham amemwambia kwamba hiyo ni jezi kama zilivyo jezi nyingine, lakini anatakiwa kuitendea haki kama ilivyo kwa wachezaji wengi waliopita ambao walivaa namba hiyo kama vile Beckham, George Best, Eric Cantona, Cristiano Ronaldo, Di Maria na wengine.
Beckham aliwahi kuivaa namba hiyo wakati anaitumikia klabu hiyo tangu mwaka 1997 hadi 2003 na aliifanyia makubwa klabu hiyo.
“Jezi namba saba inapendeza katika klabu ya Manchester United, lakini ukipata nafasi ya kuvaa jezi hiyo haina maana kwamba unatakiwa kufanya kama wachezaji ambao waliwahi kufanya miaka ya nyuma.
“Haina maana yoyote, kikubwa ni kuonesha uwezo wako wewe mwenyewe bila kujali namba ya jezi, unatakiwa kuonesha uwezo wako ukivaa jezi namba yoyote na siyo lazima iwe namba saba kama watu wanavyodhani kwa sasa katika klabu hiyo.
“Kwa upande wangu nilikuwa napenda sana kuvaa jezi namba saba, ni kwa sababu ya kumpenda Bryan Robson na Eric Cantona, lakini sijui kama niliweza kufanya vile kama wao,” alisema Beckham.
Depay alijiunga na klabu hiyo kwa kitita cha pauni milioni 25 akitokea klabu ya PSV ya nchini Uholanzi, ambapo Van Gaal aliamini kwamba mchezaji huyo ataisaidia timu kufika mbali, lakini hali imekuwa tofauti na amekuwa hana mchango mkubwa ndani ya klabu hiyo, huku mashabiki wakidai kuwa tatizo ni namba ya jezi aliyochagua haiendani na uwezo wake.