NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ameshiriki ibada ya kumuaga Mbunge wa zamani wa Kilindi mkoani Tanga, Beatrice Shelukindo (58).
Beatrice alifariki juzi Jumamosi usiku akiwa nyumbani kwa mama yake mzazi Careen Matumbo eneo la Olorieni mjini hapa alikokuwa akiendelea na matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Lowassa aliwasili katika Kanisa Kuu la Anglikan Christ Church Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), jana asubuhi akiwa ameongozana na mkewe, Regina Lowassa.
Baadhi ya viongozi wengine wa Serikali, vyama vya upinzani na chama tawala waliofika kumuaga mbunge huyo wa zamani na Bunge la Afrika Mashariki kuanzia Mwaka 2001 hadi 2004 ni mumewe, William Shelukindo, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Sophia Simba.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera, Mbunge wa zamani wa Pangani, Saleh Pamba, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Meya wa Jiji la Arusha, Calist Bukhay na Mbunge wa Korogwe, Mary Chatanda.
Akizungumza katika ibada hiyo Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Simon Makundi aliwataka waombolezaji kumtumaini Mungu na kulinda heshima aliyowapa.
Alisema kwa namna alivyomfahamu Beatrice hakuwahi kumsikia akijihusisha na vitendo vya ufisadi, badala yake aliitumikia nchi na chama chake vizuri.