Janeth Mushi, Arusha
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi kavu na majini (Sumatra), Mkoa wa Arusha, Alen Mwanry ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Arumeru kuwa gari lililopata ajali na kusababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent, halikuwa na kibali cha kusafirisha wanafunzi.
Aidha amedai mahakamani hapo kuwa kumbukumbu za Sumatra zinaonyesha kuwa gari hilo linamilikiwa na Swalehe Kiluvia ambaye si miongoni mwa washitakiwa katika kesi hiyo na kuwa lilikuwa na leseni ya kusafirisha abiria kutoka Arusha kuelekea Mererani.
Ofisa huyo ambaye ni shahidi wa nne katika kesi ya makosa ya usalama barabarani inayomkabili mmiliki wa Shule ya Msingi Lucky Vincent,Innocent Moshi na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo,Longino Nkana, ametoa madai hayo leo Mei 8, mahakamani hapo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Alice Mtenga.
“Uhalali wa leseni na matumizi ya gari lile ilikuwa kusafirisha abiria Arusha hadi Mererani na kiutaratibu magari yenye njia maalum yakitaka kusafiri njia ambayo siyo hiyo ni lazima aombe kibali,leseni tunatoa kwa mujibu wa sheria hivyo msafirishaji akibadilisha matumizi ya huduma aombe mamlaka ili apewe aliyokusudia kuifanya,” amedai.
Amedai kuhusu utaratibu wa ukaaji wa wanafunzi unatofautiana kwa maeneo ya mjini basi la wanafunzi 25 linaruhusiwa kusimamisha wanafunzi 16 ila linalosafiri nje ya mji halipaswi kuzidisha na kila mwanafunzi anatakiwa akae kwenye kiti chake na afunge mkanda.
Shahidi huyo alidai kuwa alipofika eneo la tukio kwa ajili ya ukaguzi alibaini gari hilo halikuwa la kibali cha kupita njia hiyo na kuwa hata kama gari linakodishwa kwa muda mfupi linatakiwa kufuata taratibu na kuomba kibali cha muda.
Aidha baadhi ya wazazi wa watoto 32 waliopoteza maisha katika ajali hiyo, kwa mara ya kwanza jana walihudhuria na kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo ambayo imeahirishwa hadi kesho shahidi mwingine wa Jamhuri atakapotoa ushahidi wake.