Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imeanza mazungumzo na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuangalia uwezekano wa kuirejesha michuano ya Shule za Msingi nchini UMISHUMTA na ile ya Sekondari (UMISSETA) iliyokua chimbuko la vipaji vya michezo mbalimbali kabla haijafutwa.
Hayo yamebainishwa jana Jumapili, Desemba 13, na Waziri wa Wizara hiyo huyo, Innocent Bashungwa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma.
Bashungwa amesema tayari ameshafanya mazungumzo na mwenzake wa TAMISEMI, Selaman Jafo na kwamba anataraji kuzungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kwa ajili ya kuona mpango huo unakamilika.
“Kwenye shule hizi kuna vipaji vingi ambavyo baadae vitatusaidia katika timu zetu za taifa, hivyo tutaendelea ma mazungumzo kuhakikisha michezo hii inarudi,” amesema Bashungwa.
Amesema katika timu mbalimbali wapo wachezaji wanaocheza ligi kuu wengi wamepatikana katika michezo hiyo hivyo ni muhimu kuviendeleza vipaji hivyo.
Bashungwa amesema anaamini michezo hiyo ikirudi Tanzania itakuwa tajiri wa vipaji na wengi watapata ajira.