Na MAREGESI PAUL-DODOMA
MBUNGE wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), ameishangaa Serikali kwa kushindwa kutengeneza mashine ya X-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa miezi mitano sasa.
Bashe alisema kitendo cha Serikali kushindwa kufanya matengenezo hayo hakiwezi kukubaliwa kwa sababu mashine hiyo ni muhimu kwa maisha ya wananchi wa wilaya hiyo.
Kauli hiyo aliitoa bungeni juzi alipochangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
“Katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega, hakuna mashine ya X-ray kwa sababu iliyopo imeharibika kwa miezi mitano sasa.
“Kwa kuwa tatizo ni ile Kampuni ya Phillips inayohusika na utengenezaji wa hiyo mashine, kwanini mkataba uliopo usivunjwe ili mashine itengenezwe na wengine?
“Pamoja na kwamba Serikali imeshindwa kutengeneza mashine hiyo, nampongeza sana mkurugenzi wa Wilaya ya Nzega kwa kuwasiliana na Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambayo ilikubali Emmanuel Nkusi aje kushughulikia mashine hiyo ingawa mkataba ni wa Phillips.
“Kwa sasa, Emmanuel Nkusi amechukua kifaa katika mashine hiyo ili kikatengenezwe na namuomba Waziri wa Tamisemi (George Simbachawene) asimchukulie hatua,” alisema Bashe.
Awali, hoja hiyo ya Bashe iliungwa mkono na Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi (CCM), aliyelalamikia ubovu wa mashine hiyo.
Katika maelezo yake, Zedi, alitaka Serikali iiruhusu hospitali hiyo itengeneze mashine hiyo badala ya kuitegemea Kampuni ya Phillips yenye mkataba wa kufanya matengenezo lakini haionyeshi nia ya kuitengeneza.
Wakati huo huo, idadi kubwa ya wabunge, walilalamikia uhaba wa dawa na vifaa tiba katika hospitali nyingi za Serikali.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kitendo cha hospitali za Serikali kukosa dawa na vifaa tiba hivyo, kinawakatisha tamaa wananchi ambao wanahitaji huduma kila wanapougua.
Baadhi ya wabunge hao ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Felister Bura (CCM), Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) na Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida Mohamed (CCM).