24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe afichua ufisadi wa bilioni 10/- Bodi ya Korosho

TUNU NASSOR na elias Simon-DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameitaka Bodi ya Korosho kurudisha Sh bilioni 10 zilizotolewa na Serikali kupitia Hazina  mwaka jana kununua mbolea na viuatilifu, badala yake wao wakabadilisha matumizi.

Pia ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu viongozi wote waliohusika kubadilisha matumizi ya fedha hizo zilizotakiwa kutolewa kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), lakini bodi hiyo ilizigawa na kuipa kampuni binafsi ya Bajuta International (T) Ltd.

Bashe pia ameagiza kulipwa kwa deni lililopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambalo limebaki Sh bilioni 2.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kutembelea mbolea na viuatilifu vya TFC vilivyopo katika bandari kavu tatu, Bashe alisema fedha hizo zilibadilishiwa matumizi yake na kusababisha mbolea na viuatilifu hivyo kushindwa kuwafikia wakulima.

Alisema baada ya fedha hizo kutolewa na Hazina kwenda akaunti ya Bodi ya Korosho ili zipelekwe TFC, zilibadilishwa matumizi na kupewa Kampuni ya Bajuta.

“Matokeo yake mpaka sasa mbolea na viuatilifu vilivyonunuliwa na TFC bado vimebaki katika bandari kavu tatu kwa mwaka sasa na wakulima hawakupata mbolea,” alisema Bashe.

Alisema TFC ilipatiwa barua ya mkopo (leter of credit) na BoT, yenye thamani ya Sh bilioni 7.9 ambayo hadi sasa inadai Sh bilioni 2.

“Kiutaratibu fedha hizo alitakiwa apewe TFC aweze kulipa deni la Sh bilioni 7.9 kutoka BoT ambalo alikopeshwa kabla ya fedha hizo hazijatoka, lakini Bodi ya Korosho ikaagiza Sh bilioni 4.5 kati ya bilioni 10 apewe Bajuta na Sh bilioni 4.5 iwe ‘cover’ kwake na TFC aliambulia Sh bilioni 1,” alisema Bashe.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza ndani ya siku saba Bodi ya Korosho na TFC wampelekee ripoti kuwa wametoa Sulphur na mbolea iliyokaa bandari kavu kwa mwaka sasa.

Alisema katika kipindi hicho, pia vifanyike vikao kati ya Bodi ya Korosho na TFC kujadili gharama zilizopo katika bandari kavu na nyingine.

“Mniletee orodha ya taasisi wanazodai tuweze kuomba punguzo la gharama zao ili mbolea ya NPK tani 3,000 na Sulphur tani 5,000 ziweze kutolewa humo,” alisema Bashe.

Alisema hadi sasa BoT amelipwa Sh bilioni 6 kutokana na kufanikiwa kutoa bandarini tani 2,500 hadi 3,000 ambazo baada ya kuziuza fedha zilipelekwa Bodi ya Korosho wakalipa BoT.

“Ninavyoongea hapa, Sh bilioni 10 ya Hazina imeenda, BoT anadai bilioni mbili, na Sulphur tani 5,000 bado iko bandarini,” alisema Bashe.

Aliagiza kuitwa  wataalamu wa kudhibiti ubora wakiwamo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) wakakague viuatilifu hivyo  kama bado havijaharibika ili iweze kusambazwa kwa wakulima.

“Kama kutakuwa na hasara yoyote iliyotokana na kukaa muda mrefu, hatuwezi kuiruhusu kwenda kwa wakulima na waliosababisha hasara hiyo watawajibishwa,” alisema Bashe.

Pia aliiomba Hazina kufanya uchunguzi juu ya sababu ya Kampuni ya Bajuta kupewa kipaumbele serikalini tofauti na kampuni ya Serikali ambayo ni TFC.

“Rais Dk. John Magufuli alitafuta njia ya kumsaidia mkulima kwa kutoa fedha za kununua pembejeo, fedha hizo kapewa Bajuta huku akilalamikiwa kuingiza viuatilifu visivyo na viwango,” alisema Bashe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles