Vigogo 16 wa uhujumu uchumi kulipa mabilioni

0
1042

*DPP atoa maelekezo kwa watuhumiwa

*Awataka waandike barua kwa mkono na kuiwasilisha kwa mkuu wa gereza

Kulwa Mzee-DAR ES SALAAM

 VIGOGO zaidi ya 16 wanaotuhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi ikiwemo kuisababishia Serikali hasara na kutakatisha fedha zaidi ya Sh bilioni 321 na Dola za Marekani milioni 31.5 ni miongoni mwa wanaotarajiwa kuachiwa ndani ya siku saba endapo wataomba radhi na kurejesha fedha.

Rais Dk. John Magufuli alishauri hivyo juzi.

Alisema wale wote waliokamatwa kwa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha na wapo tayari kuomba radhi na kurejesha fedha, uangaliwe utaratibu wa kuwaachia ndani ya siku saba kuanzia juzi.

VIGOGO WA IPTL

Mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Harbinder Singh Sethi na mfanyabiashara James Rugemarila wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309, 461,300158.27.

Walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza  Juni 19 mwaka juzi, hivyo wamekaa gerezani kwa zaidi ya miaka miwili.

Kesi yao inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Huruma Shaidi na upelelezi haujakamilika.

KITILYA NA WENZAKE

Aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuisababishia  Serikali hasara ya Dola za Marekani milioni 6, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Upelelezi wa kesi hiyo ulishakamilika na tayari ilishahamia Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi. Inasikilizwa na washtakiwa wako gerezani tangu mwaka juzi.

WAKILI DK. TENGA

Vigogo wa Kampuni ya Six Telecoms akiwamo Wakili wa kujitegemea Dk. Ringo Tenga wanaendelea kusota rumande tangu Novemba mwaka juzi wakikabiliwa na mashtaka sita, yakiwemo ya utakatishaji wa fedha Dola za Marekani 3,282,741.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo bado unaandaa nyaraka muhimu ili kukamilisha hatua za kuhamishia kesi hiyo Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mbali na Dk. Tenga, washtakiwa wengine ni Mhandisi na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Six Telecoms, Hafidhi  Shamte, maarufu Rashidi  Shamte, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms Limited. Wote kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 8. 

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya utakatishaji wa fedha Dola za Marekani milioni 3.2.

KISENA WA UDART

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, Septemba 13 mwaka huu ilimwondolea mashtaka manne ya kutakatisha fedha Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena (46), mke wake Florencia Mshauri, maarufu Frolence Membe (43) na wenzao watatu na kubaki na tuhuma za Uhujumu Uchumi, ikiwamo kusababisha hasara ya Sh bilioni 2.4 kwa kampuni hiyo.

Washtakiwa hao sasa wanakabiliwa na mashtaka 15 kati ya 19, ikiwamo kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia Udart hasara ya Sh 2,414,326,260.70 baada ya kuondolewa mashtaka manne ya kutakatisha fedha.

Kesi iko mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.

Washtakiwa wengine mbali na Kisena ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Chen Shi (32).

Miongoni mwa mashtaka yao wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2015 na Desemba 31, 2017 katika eneo la Jangwani, wakiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil Gas Limited, walijenga kituo cha mafuta kinachoitwa Zenon Oil and Gas katika karakana ya Kampuni ya Udart bila ya kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma na Nishati na Maji (Ewura).

Inadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam washtakiwa Robert, Kulwa, Charles na Florencia wakiwa na lengo la kuficha uhalisia, waliiba mafuta yenye thamani ya Sh 1,216,145,374 kwa kuyauza wakati wakijua mafuta hayo ni mali ya Udart.

Katika shtaka jingine, ilidaiwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 akiwa jijini Dar es Salaam kwa makusudi aliisababishia hasara Udart ya Sh 2,414, 326,260.70

Katika shtaka la mwisho, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 waliisababishia kampuni hiyo hasara ya Sh bilioni 2.4.

MALINZI NA MWESIGWA

Waliokuwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamali Malinzi (Rais), Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) na Nsiande Mwanga (Mhasibu), wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya utakatishaji fedha Dola za Marekani 173,335.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha Dola za Marekani 173,335. Awali walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 30.

Mashtaka 10 yalipungua baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Maira Kasonde kuwaona hawana kesi ya kujibu.

Washtakiwa wanajitetea baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wao.

KIGOGO TAKUKURU

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor, anakabiliwa na mashtaka nane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh bilioni 1.477.

Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Kelvin Mhina na upelelezi haujakamilika.

Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya Agosti 13, 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo huku akijua kuwa si kweli.

Katika mashtaka ya pili, inadaiwa  kati ya Januari 2012 na Mei 2017  huko maeneo ya Upanga ndani ya Wilaya ya Ilala, mshtakiwa kwa kudanganya alijipatia Sh milioni 5.2 kutoka kwa Alex Mavika ambaye ni mfanyakazi wa Takukuru kama malipo ya kiwanja  kilichopo Kijiji cha Ukuni Bagamoyo.

AVEVA NA KABURU

Aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evance Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange, maarufu Kaburu, waliondolewa shtaka la kutakatisha fedha  baada ya mahakama kuwaona hawana kesi ya kujibu.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ilifikia uamuzi huo ikiwa ni zaidi ya miaka miwili washtakiwa wakisota gerezani.

 Katika hati ya mashtaka, inadaiwa katika shtaka la kwanza,  Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Shtaka la pili la Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Marekani 300,000 kutoka akaunti ya Simba iliyoko Benki ya CRDB Azikiwe kwenda akaunti binafsi ya Aveva iliyoko Benki ya Barclays.

Shtaka la tatu linawakabilibAveva na Kaburu ambao inadaiwa kwa pamoja walighushi nyaraka iliyokuwa ikionyesha Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva kitu ambacho si kweli.

Katika shtaka la nne Aveva katika Benki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionyesha Simba wanalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000.

Shtaka la tano la kutakatisha fedha limeondolewa, Aveva alikuwa anadaiwa kuwa katika Benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za Marekani 187,817 wakati akijua zimetokana na zao la kughushi.

Katika shtaka la sita la kutakatisha fedha ambalo limeondolewa, Kaburu alikuwa anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia Dola za Marekani 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.

Shtaka la saba linawakabili Aveva, Kaburu na Hans Poppe ambao wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua kwamba si kweli.

Hata hivyo mshtakiwa Aveva na Kaburu bado wanasota rumande baada ya DPP kupinga kuondolewa kwa mashtaka ya kutakatisha fedha.

MCHUNGUZI MKUU TAKUKURU

Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyika (44), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kushawishi rushwa ya zaidi ya Sh milioni 300, kupokea na kutakatisha Dola za Marekani 20,000.

Kesi iko mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kevini Mhina.

Inadaiwa kwamba Februari 9, mwaka huu eneo la Upanga, mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru kama Mchunguzi Mkuu, aliomba rushwa ya Sh milioni 200 kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham kwa lengo la kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi zilizokuwa chini ya uchunguzi wa mwajiri wake.

Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Februari 10, mwaka huu Viwanja vya Maonyesho ya Biashara, Sabasaba vilivyopo Temeke, Dar es Salaam, alijipatia Dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Faizal Hasham kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi dhidi ya Hussein Gulamal Hasham  zilizokuwa zinafanyiwa uchunguzi na Takukuru.

MHASIBU TAKUKURU

Mhasibu Mkuu wa zamani wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo, makosa 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha jumla ya Sh 3,634,961,105.02.

Shtaka moja la kumiliki mali zilizozidi kipato halali linamkabili Gugai peke yake.

Gugai anadaiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, Gugai alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh bilioni 3.6 ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Kesi hiyo iliyopo katika hatua ya usikilizwaji, iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

MKURUGENZI OBC

Kesi nyingine ni ya kuajiri raia 37 wa kigeni wasiokuwa na vibali halali vya kufanya kazi nchini wala cheti cha msamaha, inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu ya Otterlo Business Cooperation (OBC), Isack Mollel, ambayo hadi sasa upelelezi haujakamilika.

Katika kesi hiyo, Mollel anakabiliwa na mashtaka 37, likiwamo la uhujumu uchumi.

Mollel alisomewa mashtaka 37 ya kuajiri raia wa kigeni wasio na kibali kinyume na sheria.

Anadaiwa akiwa Mkurugenzi wa OBC alitenda makosa hayo kati ya Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Kati ya mashtaka hayo 37, washitakiwa 10 pekee ndio wamefikishwa mahakamani huku wengine 27 wakiwa hawapo nchini kwani wakati shauri linafikishwa mahakamani walishaondoka.

WAFANYABIASHARA

Mfanyabiashara Mohamed Yusufali na wenzake wawili wanashtakiwa kwa kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 2,967,959,554 na dola za Marekani 12,507.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Alloycious Gonzaga na Isaack Kasanga.

Wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 45 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya sh 2,967,959,554 na dola za Marekani 12,507.

KIGOGO NIDA

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho (Nida), Dickson Maimu na wenzake, wanashtakiwa kwa uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.16.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 18, 2017.

Mbali ya Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa Nida, Avelin Momburi, Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Kaimu Mhasibu Mkuu Nida, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.

Inadaiwa kwenye shtaka la kwanza, Maimu na Mwakatumbula kati ya Januari 15 hadi 19, mwaka 2010 katika makao makuu ya Nida wilayani Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka vibaya.

Wanadaiwa kuwa waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,000 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya Nida na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8 bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya Nida kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni, waliisababishia Nida kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.

DPP ATOA MAELEZO

Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai (DPP), Bizwalo Mganga, jana alitoa mwongozo wa utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli kuhusu watuhumiwa wa makosa ya utakatishaji.

Alisema kuwa mtuhumiwa mwenyewe ambaye yupo mahabusu anatakiwa kuandika barua kupitia kwa mkuu wa gereza na kukiri kosa ndipo ofisi yake itachukua hatua.

Ofisi yake iko tayari kutekeleza ombi lililotolewea na Rais Magufuli alilowaomba juzi ma kutoa siku saba za kutubu.

“Mtuhumiwa mwenyewe ndiye anatakiwa kuandika barua na sio kuwakilishwa na wakili kwani wakili anaweza kubadilika na hata mtuhumiwa kumkana kwamba hakumtuma kufanya alichokifanya,” alisema Mganga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here