NA WINFRIDA ALEX, Mtanzania Digital
MASHINDANO ya mchezo wa Baseball ya Afrika maafuru ‘Baseball5 Africa’, yatarajia kufanyika Mei 23-26, 2022 kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Jumla ya nchi 10 zinatarajiwa kuchuana katika michuano hiyo ambapo washindi wawili wa juu watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika nchini Mexico, mwaka huu.
Mataifa yanayoshiriki ni Misri, Zimbabwe, Kenya, Uganda, Tunisia, Ghana, Bukinafaso, Zambia, Afrika Kusini na mwenyeji Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 18, 2022 katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamini, Mkapa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT), Neema Msitha, amewataka Watanzania kujitokeza kushuhudia michuano hiyo mikubwa Afrika.
“Timu ilikuwa kambini kwa muda mrefu Kibaha imemaliza ‘training’, wachezaji wana ari, wapepata sapoti pia kutoka Serikalini, tunashukuru na Baseball Afrika walisaidia kubeba mzigo kidogo lakini haijajitosheleza .
“Tunatoa wito pia kwa wadau, wadhamini makampuni, wajitokeze kusapoti kwa kuwa hii ni fursa kwa sababu haya ni mashindano ya Afrika ni makubwa yanashirikisha Mataifa mengi,” amesema Neema.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo wa Shirikisho la Baseball& Softball la Dunia(WBSC), Mattia Berardi, amesema maandalizi yanakwenda vizuri na timu kutoka mataifa shiriki zitawasili Mei 22,2022.
“Kila kitu kinakwenda vizuri kwa upande wa maandalizi na timu zitapangwa katika makundi mawili yenye timu tano tano.
“Tanzania imepangwa kundi B na Misri, Bukinafaso, Kenya na Zambia. Kundi A litakuwa na timu za Zimbabwe, Afrika Kusini, Ghana, Uganda na Tunisia.
Mashindano hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza Afrika na Tanzania ndiyo imekuwa nchi ya kwanza Afrika kupata nafasi ya kuyaandaa.