Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KINARA wa mabao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita uliofikia tamati juzi, Meddie Kagere, amesema haikuwa kazi rahisi kwake kupata mafanikio hayo kutokana na uimara wa mabeki wa timu pinzani aliokuwa anakutana nao.
Kagere alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, baada ya kupachika mabao 23.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar juzi uliomalika kwa suluhu, Kagere alisifu ushirikiano wa wachezaji wenzake kwa kusema ndio uliomwezesha kufunga mabao mengi.
“Kwa ujumla ligi ilikuwa ngumu na yenye ushindani kwani haikuwa kazi rahisi kuwamudu mabeki na kufunga mabao, unakutana na timu zenye upinzani mkubwa kiasi kwamba inakubidi utumie akili ya ziada kuweza kuwashinda,” alisema raia huyo wa Rwanda na kuongeza:
“Hakuna mechi ambayo ninaweza kusema ilikuwa rahisi, zote zilikuwa na ushindani mkubwa, kilichonisaidia ni kujituma kwangu na ushirikiano wa wachezaji wenzangu, hatua iliyonifanya nipate mafanikio haya.
“Nawashukuru mashabiki kwa kuwa pamoja katika kipindi chote na ushirikiano mkubwa waliotupa kiasi kwamba ulituongezea sana morali wachezaji.
“Ushirikiano mzuri katika timu umeweza kutusaidia kutetea ubingwa wetu kwa mara nyingine, hii ni zawadi kwao.”
Simba imetetea ubingwa wake kwa mara nyingine, baada ya kumaliza msimu ikiwa imejikusanyia pointi 93 ilizozipata baada ya kushinda michezo 29, sare sita na kupoteza mechi tatu.