31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bilionea Dar aongeza mzuka Stars

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA maarufu nchini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Motisun Group, Subhash Patel, amejitolea kugharamia kambi ya Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakayoanza Juni mosi katika Hoteli ya White Sand, Dar es Salaam.

Kambi hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya timu hiyo kuelekea  fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazoanza Juni 21, mwaka huu na kufikia tamati Julai 19, mwaka huu nchini Misri.

Taifa Stars ipo kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Kenya (Harambee Stars), ambapo itaanza kuchanga karata yake Juni 23, mwaka huu kwa kuumana na Senegal.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Walacce Karia, alisema  alimshukuru Patel  kwa mchango wake huo kwa Stars na kuwaomba Watanzania wengine kuiga mfano wake.


“Tunamshukuru ndugu yetu Patel kwa mchango wake na kuweza kusaidia michezo, kutupatia kambi katika moja ya hoteli inayomilikiwa na kampuni zake, White Sand, kwenda kuweka kambi ya siku sita, bajeti iliyokuwa itumike kwa kambi sasa itasaidia kwa mambo mengine.

“Ni vizuri watu wengine wakafuata nyayo zake na kusaidia mpira, kuwaweka kambini wachezaji katika hoteli yenye  hadhi kama hiyo ni jambo kubwa, tunamshukuru kwani  itasaidia timu yetu kuwa na morali na kufanya vizuri,” alisema Karia.

Alisema baada ya kambi hiyo ya siku sita kumazilika, kikosi hicho kitakwenda Misri Juni na kikiwa huko, kinatarajia
kucheza michezo miwili  ya kimataifa ya kujipima ubavu dhidi ya Misri.

“Timu ikiwa kule inatarajia kucheza na Misri, lakini pia tupo kwenye mchakato wa kusaka timu nyingine mbili kati ya Zimbabwe na Nigeria,” alisema Karia.

Alisema kikosi kitakachoondoka kwenda Misri kitakuwa na wachezaji 32 kabla ya kupigwa na kusalia wachezaji 23 ambao watashiriki fainali za Afcon.

Kwa upande wa Patel ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara nchini, alisema  anaamini mchango wake  utaisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika fainali hizo.

“Nafasi hii ni fahari kubwa kwa Tanzania, hivyo ni vema kuungana kwa lolote lile ambalo tunaweza kusaidia ili tuwape nguvu wachezaji, katika hoteli hiyo wanaweza kupata fursa ya kufundishwa  hata kwa kutumia komputa,” alisema.

Stars ilifuzu Afcon baada ya kuifunga Uganda mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles