KLABU ya Barcelona inajiandaa kutuma maombi kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ya kumtumia kiungo wake, Arda Turan, ili kuziba pengo la Rafinha, aliyeumia.
Barca haina uwezo wa kumtumia Turan waliyemsajili msimu huu kutoka Atlético Madrid, mpaka Januari mwakani kutokana na kifungo walichopewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa kukiuka kanuni za usajili za wachezaji vijana.
“Kitengo cha sheria kimethibitisha kuwa Fifa hawajajibu barua yao waliyotuma Ijumaa iliyopita, wakiulizia kama wataweza kumtumia Turan baada ya Rafinha kuumia… Kutokana na kutojibiwa, tumeamua tutakata rufaa kesho (jana) FIFA kabla ya kwenda mbele zaidi CAS,” ilisema taarifa ya Barca kwenye mtandao wao.
Barca kwa sasa ni ya nne kwenye msimamo wa La Liga, wakiwa wameshafungwa michezo miwili, wanakabiliwa na wimbi la majeruhi kwenye kikosi chao baada ya mastaa wao wengine, Lionel Messi na Andrés Iniesta nao kujumuishwa katika orodha hiyo.