KINSHASA, DRC
MUDA mfupi baada ya muhula wake kumalizika, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Samy Badibanga, ametangaza kuundwa kwa serikali mpya ambayo inajumuisha viongozi kadhaa wa upinzani.
Vyama vikuu vya upinzani vilitangaza vitapinga juhudi zozote za kujaribu kuongeza muda wa Rais Joseph Kabila madarakani.
Mazungumzo ambayo yamekuwa yakiongozwa na maaskofu wa Kanisa Katoliki kutafuta suluhu ya mzozo huo yanatarajiwa kuendelea leo.
Baraza la mawaziri lililotangazwa na Badibanga juzi lina mawaziri na manaibu mawaziri 67.
Kuna manaibu watatu wa waziri mkuu, mawaziri 34 wa wizara, mawaziri saba wa dola na manaibu waziri 23.
Baadhi ya mawaziri waliokuwa wanahudumu wamefutwa kazi na nafasi 20 mpya kuundwa, na kuongeza idadi kutoka 47 hadi 67.
Wakati huo huo, makabiliano kati ya waandamanaji wanaopinga kuendelea kusalia madarakani kwa Rais Kabila na maofisa wa polisi yalishuhudiwa usiku katika mji mkuu wa Kinshasa na miji mingine.