MANCHESTER, ENGLAND
KUINGO wa mshambuliaji wa klabu ya Manchester United, Paul Pogba, baada ya juzi kufanikiwa kupachika bao lake la kwanza kwa kipindi cha miezi miwili, ametumia ukurasa wake wa Instagram kutoa zawadi ya bao hilo kwa watumwa nchini Libya.
Pogba juzi alishuka dimbani kwa mara ya kwanza baada ya kukaa kwa miezi miwili akiwa majeruhi, hivyo aliweza kuifungia bao timu yake na kutoa pasi moja ya mwisho katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Newcastle kwenye Uwanja wa Old Trafford, katika michuano ya Ligi Kuu nchini England.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye ameweka rekodi ya kusajiliwa kwa kiasi kikubwa nchini humo akitokea Juventus, amedai anaguswa sana na vitendo vya ukatili ambavyo wanafanyiwa watu wa Libya, hivyo bao hilo liwe sehemu ya faraja kwao.
“Furaha yangu ni kuona narudi uwanjani tena kwa mara nyingine, lakini kwa kipindi hiki chote nimekuwa nikiwaombea wale wote ambao wanateseka na utumwa nchini Libya, nina imani kwamba Mungu atawafanyia wapesi na kuwa upande wao na hali hiyo kufikia mwisho.
Katika mchezo huo, Pogba alitajwa kuwa mchezaji bora kutokana na kila alichokifanya, hivyo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru mashabiki na wale wote ambao walimuombea aweze kurudi uwanjani mapema.
“Nawashukuru wale wote ambao walikuwa na mimi kwa kipindi chote cha kuuguza tatizo langu la nyama za paja, nawashukuru kwa dua zenu na sasa nipo fiti kwa ajili ya kuitumikia klabu yangu kwenye michuano mbalimbali.
“Kikosi hiki kitakuwa kwenye ubora wake kwa kuwa mimi nimerudi uwanjani, Zlatan Ibrahimovic amerudi na Marcos amerudi uwanjani, tuna furaha sana, nilikuwa naumia sana wakati nipo nje huku nikiwa na lengo la kutaka kuisaidia timu lakini nashindwa kutokana na hali yangu.
“Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwa kuwa ni mapema kusema lolote baya, kila mmoja anapigania ili kumaliza msimu vizuri, hivyo kwa upande wetu bado tuna nafasi hiyo ya kufanya vizuri,” aliongeza.
Kocha wa klabu hiyo, Jose Mourinho, ameweka wazi kuwa anatarajia kumpumzisha kiungo huyo kwenye mchezo dhidi ya FC Basel, keshokutwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi.
Hadi sasa United imefanikiwa kushinda michezo minne katika hatua hiyo na sasa inahitaji pointi moja kuweza kufuzu kwenye hatua ya mtoano