BERLIN, UJERUMANI
BALOZI mpya wa Marekani nchini Ujerumani, Richard Grenell amezua utata baada ya kuwaponda viongozi wa Ulaya pamoja na kueleza nia ya Marekani kusaidia vuguvugu zinazopinga tawala barani Ulaya.
Kauli hiyo iliyoikasirisha Ujerumani ilionekana baada ya tovuti ya habari inayoelemea siasa za mrengo wa kulia ya Breitbart kuweka mahojiano iliyofanya na balozi huyo mpya.
Kuna wanaotaka Richard Grenell, afukuzwe Ujerumani kwa kuingilia mambo ya ndani pamoja na kutoa matamshi ya kichochezi na yenye kuwagawa watu.
Katika mahojiano hayo, balozi huyo aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Marekani, Donald Trump alieleza nia yake ya kuwezesha vuguvugu zinazopinga tawala zilizozoeleka barani Ulaya.
Vipengele vyake vingi katika mahojiano hayo vitawafurahisha wanachama wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia – maarufu kama chama mbadala kwa Ujerumani (AfD).
Balozi huyo pia aligusia suala la wananchi wengi wasio na sauti, ruzuku ya Serikali kwa wafanyakazi wa kiwango cha wastani.
Aidha, alikosoa sera za Ujerumani kuhusu wakimbizi na aliwaeleza wanasiasa wa Ujerumani kuwa waliopitwa na wakati.
Si mara ya kwanza kwa Grenell kuingilia mambo ya ndani ya Ujerumani.
Muda mfupi baada ya kuteuliwa, aliitaka Ujerumani isitishe biashara na Iran kutokana na mzozo unaoendelea kuhusu makubaliano ya nyuklia na Iran.
Ni kitu kisicho cha kawaida kwa balozi kuingilia mambo ya ndani ya mwenyeji wake.
Ilivyozoeleka, wadhifa huo unatumiwa kujenga uhusiano ya kidiplomasia na kusuluhisha migogoro.
Lakini wale ambao wameshangazwa na tabia za Grenell bado hawajaelewa kuwa kwa vile Trump yu Ikulu ya Marekani, kila kitu- ikiwamo diplomasia kimebadilika.
Wachambuzi wa mambo wanasema kauli ya Hrenell inaakisi mwenendo wa Trump kwa kuunga mkono kile ambacho kitawapa umaarufu zaidi ikiwamo siasa za kizalendo ambazo zinaenea kwa kasi Ulaya.
Kwa kufanya hivyo, Trump na timu yake wanaamini wataudhoofisha Umoja wa Ulaya na hivyo kutoa nafasi kwa Marekani kunufaika.