24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

USAFIRI WA MWENDOKASI KUSUKWA UPYA (4)

Na BAKARI KIMWANGA-DAR ES SALAAM


AZMA ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi kwa wananchi wake, jambo ambalo linachagizwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka, ambao upo chini ya Wakala wa DART, umekuwa ukisimamiwa, ingawa bado changamoto kadhaa zimekuwa zikiibuliwa na wananchi, hasa wanaotumia huduma hiyo.

Pamoja na hali hiyo, bado kero ya ubovu wa mabasi ambayo yamekuwa yakiharibika kila wakati pindi abiria wanapokuwa safarini limekuwa ni jambo la kawaida kwa sasa.

Mabasi hayo, ambayo yapo chini ya Kampuni ya Ubia ya UDART, ambayo ni Kampuni tanzu ya Simon Group, kila mara hueleza ubovu huo huchangiwa na mafuriko ambayo husababisha kuharibika kwa magari hayo.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umebaini kuwa, UDART wana magari machache katika uendeshaji wa mradi huo na hata yaliyoletwa bado mengine ni mabovu.

Licha ya hali hiyo, pia hata matengenezo ya uhakika wa magari hayo kwa sasa umekuwa wa kusuasua, hali ambayo ni hatari kwa usalama wa abiria wanaotumia usafiri huo.

Baada ya jana kuona namna ‘mchwa’ wanavyotafuna fedha za walipa kodi vituoni na hata kuibuka kwa mwingiliano katika ukusanyaji wa fedha kati ya UDART na Maxcom, leo tunaangazia ubovu wa mabasi hayo ambayo huzima njiani na hata kuwa na matairi vipara.

Kutokana na ubovu huo wa mabasi hayo, wakati mwingine huwafanya watu kukaa vituoni kwa zaidi ya saa mbili, huku wengine wakilazimika kuingia katikati ya barabara za mwendokasi ili waletewe mabasi hayo.

UWADAR WATAKA MRADI

Umoja wa Wasafirishaji Abiria Mkoa wa Dar es Salaam (UWADAR), wanasema wako tayari kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka iwapo mwendeshaji wa sasa atashindwa.

Kauli hiyo ya UWADAR imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa, kusema kuwa, serikali inatafuta mbia mwingine atakayeshirikiana na mwendeshaji wa sasa ili kuongeza changamoto.

Alisema iwapo mwendeshaji wa sasa ataonekana kushindwa kuuendesha mradi huo, watamwondoa.

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa UWADAR, Kismat Jaffar, alisema wao wako tayari kuendesha mradi huo kwa kuwa wana uzoefu katika masuala ya usafirishaji.

“Tumefarijika na kauli ya Waziri Mkuu kwa kuwa ndio kilio chetu cha muda mrefu tukitaka kuendesha mradi huu,” alisema Jaffar.

Jaffar alisema iwapo watapatiwa kuuendesha mradi huo, watashusha nauli kutoka Sh 1,050 hadi Sh 700 kwa abiria wanaotoka Mbezi kwenda Kariakoo na Feri, kwani wanajua mwendeshaji wa sasa ana taarifa nyingi zinazotia shaka, inakuwaje anayepata hasara bado anafanya kazi.

“Huwezi kujaza watu kwenye magari kiasi kile tena unawatoa shilingi 650 kwa kila safari, kisha unasema unapata hasara. Halali kabisa hata shilingi 500 kwa kila safari anapata faida kubwa na tunajua mapato anayokusanya kwa siku ni mamilioni ya shilingi anakusanya,” alisema.

Alisema iwapo watapewa kazi hiyo, watatumia mfumo unaotumiwa na UDART, lakini mabasi yao yatakuwa na injini ya mbele, yatakayotumia gesi.

“Tutatumia gesi katika magari yetu ambayo tutayaleta kwa kuwa nchi ina gesi ya kutosha,” alisema Jaffar.

Alisema tayari wana kampuni ya usafirishaji na pia kuna watu waliokuwa tayari kuwafadhili kupata mabasi, wakiwamo Benki ya Dunia (WB) na nchi ya China.

Alisema iwapo watapewa mradi huo, hali itabadilika haraka na wananchi watasahau adha wanayoipata kwa sasa.

“Sisi watupe miezi sita tu ya majaribio na kama tutashindwa itajulikana, kwa kuwa hatutaondoa daladala za kawaida na abiria watachagua usafiri wanaotaka kutumia,” alisema Jaffar.

WAKUMBUSHA BIL. 2/-

Alisema wana mtaji wa Sh bilioni mbili ambazo waliziingiza kama hisa katika mradi wa kuanzisha Kampuni ya UDART, japokuwa hadi sasa hawajawahi kupewa gawio la hisa hizo.

“Katika mkataba wake, UDART alilazimika kutushirikisha wasafirishaji wa Dar es Salaam, ambapo alitukata shilingi  milioni moja kwa kila gari alizoziondoa barabarani na hivyo kukusanya Sh bilioni mbili ambazo anazifanyia kazi kwa miaka miwili, lakini mpaka leo hatujapata gawio,” alisema Jaffar.

Aliongeza kuwa, pamoja na UDART kutangaza kupata hasara kila mwaka, lakini wao wanajua anapata faida kiasi gani kwa siku.

“Tunajua anapata faida kiasi gani, kwani kwa siku gari moja linaingiza zaidi ya Sh milioni moja, hivyo ndani ya miezi mitatu inalipa gharama za manunuzi ya basi hilo na kuendelea kuingiza faida,” alisema Jaffar.

Alisema hata hivyo, mradi huo ulikuja mahsusi kuwasaidia wasafirishaji wa jiji la Dar es Salaam, lakini mambo yakawa ndivyo sivyo.

“Mwendeshaji wa sasa alikuja kwa nembo ya UDA baada ya kununua hilo shirika, lakini hakuwa na uzoefu wowote wa masuala ya usafirishaji, ndiyo maana ametufikisha hapa,” alisema Jaffar.

SUMATRA, TRAFIKI

Hatua ya uwepo wa usalama wa magari hayo MTANZANIA ilizungumza na Mkurugenzi wa Barabara wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra),  Johansen Kahatano, ambaye alisema suala la ukaguzi hufanywa moja kwa moja na Jeshi la Polisi, ingawa nao sasa wanalazimika kufuatilia kwa karibu usalama wa mabasi hayo ya mwendokasi.

“Suala la ukaguzi hufanywa na wenzetu wa Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani (trafiki), ila kwa hili la matairi vipara tutalifuatilia ili kujua ukweli wa mabasi haya,” alisema Kahatano.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Malson Mwakyoma, alisema hawezi kusema matairi ya mabasi ya mwendokasi yamekwisha mpaka wafanye ukaguzi wa kuangalia tarehe ya kutengenezwa na ukomo wa matairi hayo.

Alisema watu wengi huangalia tabaka la juu kama kigezo cha kuisha kwa matairi ya gari husika, badala ya ubora wa tairi lenyewe.

“Suala la kuwa kipara tunachosoma sisi ni tairi ilitengenezwa lini na ‘expire date’ yake ni lini, kila tairi imeandikwa, sasa wengi huwa wanasema matairi yamekwisha kwa kuangalia tu kashata ya tairi, sasa siwezi kuhukumu kwa kusema matairi ya mwendokasi yamekwisha mpaka tufanye ukaguzi,” alisema Mwakyoma.

Alisema kwa mabasi ya mwendokasi, wanatumia utaratibu wa wamiliki wa mabasi hayo kuwaomba polisi wakakague au polisi kuwaomba wamiliki kupeleka magari yakakaguliwe.

Alisema kuhusu magari kuharibika ni matatizo ya mfumo ambayo yanaweza kutokea hata kama gari hilo limetengenezwa siku hiyo ambapo mara nyingi huhusisha mfuo wa umeme wa gari, breki au injini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,853FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles