32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI SEIF VAT ITAZAMWE UPYA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MAKAMU wa Pili Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema ipo haja kwa serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  kuangalia uwezekano wa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wawekezaji wa sekta ya makazi hapa nchini.

Amesema kuondolewa kwa VAT kutarahisisha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi.

Balozi Iddi aliyasema hayo mwishoni mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizindua mradi mkubwa wa nyumba za makazi unaofahamika kwa jina la Hamidu City Park uliopo Wilaya ya Kigamboni.

Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Orange Tanzania Limited na unalenga kujenga nyumba za kisasa zaidi 1,560.

“Makazi bora ni haki ya kila Mtanzania hivyo sisi kama serikali ni wajibu wetu kila siku kufikiria sera bora zitakazo wawezesha wananchi kufanikisha hilo.

“Kuna haja ya taifa kuwekeza zaidi kwenye mipango miji inayowaunganisha watanzania badala ya ile inayowatenganisha kulingana na vipato vyao.

“Sifa ya miji mizuri ni pamoja na muingiliano wa kimakazi kati ya watu wenye vipato tofauti. Hatuhitaji kuwa na miji inayowatenganisha watu,” alisisitiza Balozi Iddi

Wakati huo huo Balozi Iddi alizindua nyumba 20 za awali za mradi huo na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwekeza kwenye mradi wa ujenzi.

Alimuahidi Mkurugenzi Mkuu Kampuni ya Orange Tanzania Limited, Hamidu Mvungi kuwa atamuunga mkono kwa kununua nyumba moja katika mradi huo.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Orange, Hamidu alisema mradi huo unahusisha eneo la ekari zaidi ya 130 na utatekelezwa kwa awamu tano tofauti.

“Awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa nyumba zaidi ya 150 ambazo zitauzwa kati ya Shilingi milioni  120 hadi  370. Tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kupunguza kama siyo kuondoa kabisa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la bei kwenye nyumba za makazi,” alisema Hamidu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles