MSHAMBULIAJI wa timu ya Real Madrid na timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale, jana alitajwa kuwa katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Ballon d’Or ya mchezaji bora wa mwaka 2016.
Tuzo hiyo inayotolewa kila mwaka, pia ilimtaja mshambuliaji mwingine wa Madrid, Cristiano Ronaldo, kuwania mwaka huu pamoja na mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang na kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon.
Kwa mujibu wa jarida la France Football linaloandaa tuzo hiyo, limewataja jumla ya wachezaji 30 katika kinyang’anyiro hicho na kutarajia kuwapunguza wachezaji watano kila baada ya saa mbili kuanzia jana.
Tuzo hiyo imekuwa ikitolewa na jarida hilo kila mwaka tangu mwaka 1956, lakini kwa miaka sita ya hivi karibuni ilikuwa ikitambulika kama Fifa Ballon d’Or kutokana na ushirikiano uliokuwapo na Bodi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa.
Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi, alishinda tuzo hiyo mwaka uliopita na kuweka rekodi ya kushinda mara tano.
Mara ya mwisho mchezaji aliyeshinda zaidi ya Messi au Ronaldo ilikuwa mwaka 2007 wakati aliyekuwa mchezaji wa AC Milian, Ricardo dos Santos ‘Kaka’ kushinda tuzo hiyo.
Wachezaji watano wa Ligi Kuu England waliowahi kutajwa katika tuzo hiyo ni mchezaji wa Manchester City, Yaya Toure, Aguero na Kevin de Bruyne na Arsenal, Alexis Sanchez na Chelsea,  Eden Hazard.
Wakati wachezaji wa Manchester United ni Paul Pogba na Zlatan Ibrahimovic ambao wamejumuishwa kabla ya kujiunga na timu hiyo.