24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

BADO TUNA MENGI YA KUJIFUNZA KENYA

NA FARAJA MASINDE

MAPEMA wiki hii Mahakama ya Juu nchini Kenya ilitangaza kukubali muungano wa upinzani (NASA) kupekua seva zilizotumiwa na Tume ya Uchaguzi Mkuu nchini humo (IEBC), kwa ajili ya kujiridhisha na matokeo yaliyompa ushindi Rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

Hili ni jambo la kupongezwa na linalopaswa kuigwa na Tanzania, kwani Kenya imeweka uwazi kwa chama chochote ambacho kina shaka na ushindi kuchukua hatua ambazo kinaamini kuwa ni sahihi ikiwamo maandamano, kufungua kesi mahakamani na hata kuomba kupitiwa na kuangaliwa upya kwa mfumo uliohusika.

Jambo hilo naweza kusema kuwa limekuwa ni nadra kuliona kwa nchi nyingi za Kiafrika, hata wapinzani wanapodai haki zao wamekuwa hawapewi ushirikiano wanaopaswa kupewa ikiwamo kuzuiwa kwenda mahakamani kupinga matokeo ya kiti cha urais.

Na pia inatoa picha kwamba vyama hivyo vina imani na chombo hicho cha juu cha uamuzi na kwamba wanatarajia kupata haki kwenye madai yao hayo ya msingi waliyoyawasilisha mahakamani.

Kwa maana nyingine ni kwamba Katiba ya Tanzania imekuwa haitoi nafasi ya vyama vya siasa kupinga au kuhoji matokeo ya kiti cha urais mahakamani, jambo ambalo kwa nyakati hizi tulizonazo halina budi kufanyiwa marejeo upya kwenye Katiba yetu.

Kinyume cha kutumia nguvu nyingi katika kudhibiti upinzani, kushindwa kujiridhisha na matokeo husika yanayotangazwa.

Pia mbali na hilo, kama Taifa tunahitaji kuwa na tume huru ambayo haifungamani na chama chochote kilichoko madarakani kama ambavyo tumeshuhudia kwa wenzetu wa Kenya, hii inakuwa ni rahisi hata kutoa ushirikiano kwa wagombea pindi inapotokea wameshindwa kinyume na kuwa chini ya chama tawala, ambapo kamwe haiwezi kutoa nafasi kwa upinzani kuweza kujiridhisha na matokeo husika kwa kuhofia kupoteza vibarua vyao.

Kwani kama mambo yatafanyika kwa ukweli na uwazi, kamwe hakutakuwa na haja ya kukosa uhuru kwa wagombea wa upinzani, kwani demokrasia ya kweli hahitaji chuki au kukosekana kwa haki, badala yake, inahitaji amani na uwazi ikiwamo kutoa haki ya kufanya maandamano kwa pande zote.

Mwarobaini wa kupiga hatua hii kama ambavyo wameweza kufanikiwa kwa wenzetu wa Kenya, ni katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na Katiba mpya ambayo itaweza kuzingatia haya yote ikiwamo kutoa uhuru wa matokeo ya uchaguzi wa urais kuhojiwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles