29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Babake Mo afunguka

Na NDREW MSECHU

MFANYABIASHARA Gullamhusein Dewji, ambaye ni baba wa mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo), amezungumzia juu ya kutekwa kwa mtoto wake akisema mpaka sasa hajapata taarifa zenye kutia matumaini.

Gullamhusein hajawahi kuzungumzia tukio hilo tangu litokee wiki iliyopita, kwani hata alipojitokeza mbele ya vyombo vya habari kutangaza dau la Sh bilioni moja kwa mtu atakayetoa taarifa za kuwezesha kupatikana kwa mtoto wake, aliyezungumza kwa niaba ya familia ni Azim Dewji ambaye ni mjomba wa Mo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Gullamhusein alisema familia inaendelea kufanya dua, lakini bado hawajapata taarifa yoyote ya kuwapa matumaini kuhusu alipo Mo ambaye alitekwa na watu wasiojulikana Oktoba 11, mwaka huu.

“Hadi sasa hatuna taarifa yoyote inayoweza kutupa matumaini ya kupatikana kwake, tunaendelea kufanya sala tu na tunaomba wananchi watupe ushirikiano wa kumpata kijana wetu,” alisema.

Kufungwa biashara za METL

Kuhusu taarifa iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL) zitafungwa, Gullamhusein alikanusha taarifa hizo.

Mtanzania ilipomuuliza juu ya ukweli wa taarifa hizo, alisema. “Siyo kweli, hakuna kitu kama hicho,” alisema.

Polisi: Tunafuatilia kila taarifa

Kamnda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alipoulizwa hatua iliyofikia kwenye kuchunguza tukio hilo, alisema bado wanafanya oparesheni hiyo ambayo inaendelea kuwa ngumu.

Taarifa ambazo MTANZANIA imezipata kupitia kwa vyanzo vyake, zinaeleza kuwa vyombo vya usalama vimekuwa vikiendelea kufuatilia tukio hilo kwa kuchunguza kamera za CCTV zilizoko maeneo ya jirani na Hoteli ya Colosseum.

Moja ya chanzo chetu kilieleza kuwa baadhi ya picha zimeonyesha mwenendo wa gari linalodhaniwa kuwa ndilo lililokuwa limembeba Mo.

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa itakuwa ni kuingilia upelelezi, suala ambalo kwa utaratibu halitakiwi kwa sasa.

Alisema kutokana na operesheni maalumu ya kumpata Mo inayoendela kwa sasa, wanafuatilia kwa karibu kila taarifa wanayoipata na kuona iwapo inaweza kusaidia kupatikana kwake.

“Ni kwamba kwa sasa tunafanya kazi muda wote, tumepata taarifa kadhaa ambazo tumekuwa tukizifuatilia tunafika mahala tunaishia hewani.

“Tunaendelea kutafuta njia, ndiyo maana unaona kazi inakua ngumu, ila tunafuatilia kila taarifa tunayoona inaweza kutusaidia, hatuachi taarifa yoyote hewani,” alisema Mambosasa.

Alisema polisi inahitaji muda wa kufuatilia kwa undani na kujiridhisha katika uchunguzi wake wa kipelelezi unaoendelea kwa sasa katika maeneo yote yanayodhaniwa kuw ayanaweza kuwezesha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Bilioni moja

Oktoba 15, akizungumza na waandishi wa habari Msemaji wa familia hiyo Azim Dewji, alisema wamefikia hatua hiyo ili kuongeza juhudi za kuhakikisha mtoto wao anapatikana mapema.

“Familia inaahidi kwamba mtoa taarifa pamoja na taarifa zitabaki kuwa za siri baina ya mtoa taarifa na familia,” alisema Dewji.

Alisema wanapitia katika kipindi kigumu na kuwaomba watu mbalimbali waendelee kuwaombea. “Tunaishukuru Serikali na taasisi zake kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha mtoto wetu anapatikana.

“Tunavishukuru vyombo vya habari kwa kazi kubwa ya kuutaarifu umma jambo hili zito.

“Tunashukuru taasisi za dini na kila mmoja wenu kwa maombi na kutufariji katika kipindi hiki kigumu familia inachopitia. Tunaomba muendelee kutuombea,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa mwenye taarifa awasiliane nao kupitia Murtaza Dewji kwa namba 0755030014, 0717208478, 0784783228 au kupitia barua pepe [email protected].

Mo alitekwa nyara alfajiri ya Oktoba 11 alipokuwa akiingia katika kituo cha mazoezi cha Hoteli ya Colloseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam na hadi leo, ikiwa ni siku ya nane bado hajapatikana.

Biashara za Mo

Biashara zake zinachangia asilimia 3.5 ya pato la Taifa na hapa Tanzania kampuni zake zinatoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 23,000.

Katika umri wa miaka 43 Mo ametangazwa na Jarida la Forbes kuwa bilionea kijana kuliko wote Afrika akimiliki mali inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh trilioni 3.5.

Utajiri wake unatokana na kutawala sekta mbalimbali na kuliteka soko la bidhaa za walaji kama vile vyakula kiasi cha kushika namba moja kati ya kampuni binafsi zinazoongoza kwa kuajiri watu wengi.

Hata hivyo haijapata kuwapo tetesi au ripoti yoyote rasmi inayoonyesha kuwa shughuli zake za biashara zinaweza kumzalishia maadui kiasi cha kuamua kumteka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles