HASSAN DAUDI NA MITANDAO
SERIKALI ya Afghanistan chini ya Taliban inajaribu iwezavyo kuficha ukweli. Haitaki kukiri kuwa iko kwenye vita nzito ya kupambana na wanamgambo wa Dola ya Kiislam (IS). Inachojaribu Taliban ni kudanganya ulimwengu kwa kukanusha kuwa hakuna IS ndani ya nchi yao. Wamegoma kukubaliana na ukweli kwamba IS ni wapinzani wapya baada ya kuyashinda majeshi ya Marekani na Jumuhiya ya Kujihami ya nchi za Ulaya (NATO).
Duru za kisiasa zinaonesha tofauti iliyojitokeza na kusababisha mvutano kati ya makundi mawili hayo. Ni kwamba kila upande hauuoni mwingine katika taswira nzuri. IS wanawachukulia Taliban kuwa si wenye msimamo mkali wa Dini, kama ambavyo nao wanaonekana wasaliti.
Pande mbili hizo pia zinatofautiana linapokuja suala la malengo. Wakati shabaha ya Taliban ikiwa ni kusimamisha utawala wa Kiislam ndani ya Afghanistan, IS wao wanataka watikise dunia, wawe tishio kwa kila taifa litakaloingia kwenye anga zake.
Wakati uongozi wa Taliban ukiendelea kuficha kilichoko sasa, mamia ya raia wa Afghanistan wanaendelea kupoteza maisha kutokana na mashambulizi ya IS. Miili ya watoto, wanawake na wazee inaendelea kuokotwa barabarani. Hali si shwari, hasa Mji wa Kaskazini mwa Afghanistan, Jalalabad. Ni kawaida watu kupigwa risasi, kunyongwa si mageni eneo hilo na watekelezaji ni hao hao, IS.
Hakuna siri kuwa ni IS ndiyo waliotekeleza shambulio la bomu miezi miwili iliyopita katika Uwanja wa Ndege wa Kabul na kuua watu zaidi ya 150. Kwa ufupi, mbinu za kushambulia na kutokomea walizokuwa wakitumia Taliban kuyapa mateso majeshi ya kizungu (Marekani na NATO) ndizo hizo hizo walizonazo IS.
Licha ya yote hayo, kwa Dkt. Bashir, ambaye ndiye kiongozi wa idara ya usalama ya Taliban katika Jimbo la Nangarhar jijini Jalalabad, wala haoni kama IS ni tishio, hasa mbele ya Taliban. Dkt. Bashir anapinga kwa nguvu zote taarifa zinazodai kuna IS ndani ya Afghanistan.
Akiwa kwenye vyombo vya habari, mara zote utamsikia Dkt. Bashir akisema hakuna vita inayoendelea Afghanistan na nchi hiyo iko salama kabisa chini ya utawala wa Taliban. Mbaya zaidi, anadai kuna Kundi linaloitwa IS katika nchi yao, Afghanistan. “Jina ‘Daesh’ (wanalotumia IS) linamaanisha Syria na Iraq,” anasema na kuongeza: “Hakuna kikundi kinachoitwa Daesh hapa Afghanistan. Ni kikundi cha wasaliti tu, ambacho kinapingana na Serikali yetu ya Kiislam.”
Ukipishana na kauli ya kiongozi huyo, utabaini kuwa IS wako kwenye ardhi ya Afghanistan tangu mwaka 2015 lakini vikosi vya Marekani na NATO vilivyokuwa nchini humo viliwadhibiti kwa kiasi kikubwa, kabla ya kupata nguvu walipotoroka jela baada ya wazungu hao kuondoka.
IS wamekuwa wakitelekeza mashambulio mengi, hasa tangu Taliban walipochukua nchi miezi michache iliyopita. Kama utakumbuka, mwanzoni mwa mwezi huu tu, walishambulia kwa bomu msikiti wa waumini wa Kiislam wa Dhehebu la Shia ulioko Mji wa Kaskazini, Kunduz, kabla ya kufanya hivyo Kandahar, moja ya maeneo ambayo Taliban wamekiti mizizi.
Kama itafaa kukumbusha, mwanaharakati wa haki za kiraia, Abdul Rahman Mawen, alipigwa risasi na wapiganaji wa IS, tukio lililoshuhudiwa na watoto wake wadogo aliokuwa nao kwenye gari wakirejea nyumbani baada ya kuhudhuria sherehe ya harusi. IS walikiri kuhusika na unyama huo.
Hayo yote hayaonekani kumshitua Dkt. Bashir na hatimaye kukiri tishio la IS na badala yake anasema: “Tunaiambia dunia, isiwe na hofu. Kama kikundi kidogo tu cha wasaliti kinaibuka na kufanya mashambulizi, kwa uwezo wa Mungu, kama tulivyoushinda mkusanyiko wa nchi 52 (Marekani na wenzake), basi nacho kitapigwa tu.”
Huku Dkt. Bashir akitoa kauli za kishujaa hizo, bado hofu ya IS kutanua mbawa na kutekeleza mashambulizi mengi zaidi imetawala sit u kwa raia wa Afghanistan, bali hata kwa majirani zao. Kwa mujibu wa maofisa wa Marekani, ndani ya miezi sita ijayo au mwaka, IS walioko Afghanistan watakuwa wamekua na kufikia uwezo wa kupeleka mashambulia yao kwa nchi zingine za nje.
Marekani wanaiona hatari hiyo kipindi hiki ambacho IS haijashikilia hata jimbo moja (baada ya kukimbizwa Nangarhar na Kunar), ina wapiganaji wachache, huku Taliban ikijivunia wanajeshi 70,000 waliopewa mafunzo na silaha za kisasa na Marekani.
Hata hivyo, wasiwasi ni kwamba idadi ya wapiganaji wa IS haitabaki kama ilivyo na badala yake itaajiri wengine kutoka nje ya Afghanistan, hasa Pakistani. Pia, nguvu yao inaweza kuimarishwa na wanajeshi watakaona hawana nafasi au wanapuuzwa ndani ya Serikali ya Taliban.