29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Baada ya kuwashindwa Waarabu Yanga sasa yapangiwa Waangola

MMG25771*Pluijm asema mapambano yanaendelea

CAIRO, MISRI

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC wanatarajia kukutana na Sagrada Esperanca ya nchini Angola katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutupwa nje ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Washindi nane wa michezo ya Kombe la Shirikisho watapambana na wale nane ambao wamepoteza michezo yao katika klabu bingwa, klabu hizo za Shirikisho ni Esperance (Tunisia), Stade Gabesien (Tunisia), FUS Rabat (Morocco), Misr Makkassa (Egypt), Esperanca (Angola), CF Mounana (Gabon), Kawkab (Morocco) na Medeama (Ghana).

Wakati huo zile zilizopoteza klabu bingwa ni TP Mazembe (DR Congo), Etoile du Sahel (Tunisia), El Merreikh (Sudan), Stade Malien (Mali), MO Bejaia (Algeria), Ahli Tripoli (Libya), Mamelodi Sundowns (South Africa) na Young Africans (Tanzania).

Yanga ambao walikuwa wanatafuta tiketi ya kuingia hatua ya robo fainali, walitolewa na Al Ahly kwa jumla ya mabao 3-2 nyumbani na ugenini. Katika mchezo wa nyumbani Yanga ilifanikiwa kutoka sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati mchezo wa marudiano ambao ulipigwa juzi kwenye Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria, Misri, ilikubali kichapo cha mabao 2-1.

Sasa Yanga inakutana na klabu hiyo ambayo inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi nchini Angola baada ya kucheza michezo sita.

Mabingwa wa Afrika msimu uliopita TP Mazembe waliovuliwa ubingwa na Wydad Casablanca ya nchini Morocco, wao watapambana na klabu ya Stade Gabesien ya nchini Tunisia, ambayo inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi kwa sasa.

Wababe wa Azam FC, Esperance ya nchini Tunisia wanatarajia kukutana na MO Bejaia ya nchini Algeria ambayo inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi.

Michezo mingine katika ratiba hiyo ni Stade Malien (Mali) dhidi ya FUS Rabat (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia) ikicheza na CF Mounana (Gabon), Ahli Tripoli (Libya) dhidi ya Misr Makassa (Egypt), huku El Merreikh (Sudan) ikicheza na Kawkab (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) itapambana na Medeama (Ghana). Michezo ya kwanza itapigwa Mei 6 na 8 mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema kuwa bado mapambano yanaendelea kuhakikisha klabu yake inakuwa tishio Afrika.

Kuhusu kutolewa kwao na Al Ahly, Pluijm alisema hawezi kuongelea sana mchezo huo kwani tayari umepita.

“Siwezi kuzungumzia sana mchezo huu wala michuano hii tena, ila lazima malengo ya kuhakikisha Yanga wanakuwa bora Afrika yatimie kwani tumerudi Kombe la Shirikisho.

“Ninachoweza kusema ni pongezi kwa wachezaji wangu wote tumepambana na kuonyesha kiwango chetu cha hali ya juu, nadhani timu zote tulizoweza kucheza nazo katika michuano hii mwaka huu zitatukumbuka,” alisema Pluijm.

Naye ofisa habari wa klabu hiyo, Jerry Murro, alisema kuwa baada ya kutolewa katika michuano hiyo, leo wanatarajia kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Jumapili  katika Uwanja wa Mkwakwani.

“Tupo njiani na tunatarajia kutua usiku (jana), hivyo wachezaji wote wako salama tunajiandaa kwa ajili ya mchezo wa FA,” alisema Muro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles