25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

BAADA YA GESI, TUSUBIRI ‘VITA’ YA ARDHI

Na Markus Mpangala


KILIO cha gesi yetu kimesikika tena na safari hii mzungumzaji ni Rais Dk. John Magufuli ambaye amekaririwa na vyombo vya habari kuwa umiliki wetu katika gesi asilia ni asilimia 30 pekee.

Suala la gesi hunikumbusha migogoro ya ardhi iliyotamalaki kila kona ya nchi. Kuna vilio vya uporwaji wa ardhi na wananchi hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa uwekezaji na umilikaji ardhi.

Tumesikia mara kadhaa kuona jinsi wananchi wanavyohamishwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.  Sitashangaa miaka miwili ijayo wananchi wa Kijiji cha Ndumbi, Kata ya Mbaha katika tarafa ya Ruhuhu wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma wakihamishwa huku ardhi yao ikitumika kwa uchiambaji wa Makaa ya Mawe.

Suala la uwekezaji katika nchi yetu inabidi wananchi wawekewe kipaumbele katika umilikaji wa ardhi ili kuepusha mapigano. Ndani ya nchi yetu kuna migogoro baina ya wilaya na wilaya nyingine kuhusu mipaka na ardhi.

Kuchipua kwa hayo yote ni kutokana na kuzembea kuzingatia kanuni ya msingi ya uwekezaji na maendeleo. Hakuna maendeleo yanayopatikana bila misingi na vipaumbele.

Kama leo unaweka mbinyo katika kujipatia pato ikiwemo kuwanyang’anya ardhi wananchi, bila shaka tunatengeneza taifa la wahalifu. Miongoni mwa unyang’anywaji wa ardhi ni kusingizia ukodishwaji kwa wawekezaji.

Kiuhalisia hakuna uhusiano mzuri kati ya wenyeji (wananchi) na wawekezaji. Sababu kubwa ni mtazamo hasi walionao baadhi ya wananchi unaotokana na kushindwa kuwaelimisha juu ya haki za ardhi au haki zake kumomonyolewa.

Uwekezaji unavyoshamiri, ndivyo majukumu ya baadhi ya wananchi yanavyopungua, ardhi inavyouzwa na haki ardhi inavyotoweka.

Endapo tutazingatia misingi kwamba kuweka vipaumbele wananchi wamiliki ardhi yao kwa haki na kuwa haki ya msingi kwa mujibu wa Katiba, bila shaka tutaepusha kadhia hii ijayo.

Wakati watu wanatafuta mkate na maji, wanahitaji ardhi. Kama ardhi yao imechukuliwa huku fidia ikipigwa danadana isifike mahali tukasema wananchi ni wachochezi.

Bara la Afrika linaongoza kwa uuzwaji wa ardhi. Wawekezaji wananunua ardhi Afrika kwa bei rahisi, huku kiwango chetu cha usimamizi kikishuka siku hadi siku.

Wakulima wadogo ambao ndio msingi wa kilimo  afrika na wenye kuishi kwa mtindo wa makundi yenye uhusiano mzuri na kumiliki ardhi kwa mitindo ya jadi wapo kwenye hatari ya kukosa ardhi.

Ununuzi wa ardhi umechukua nafasi Afrika huku makampuni ya kigeni yakisonga mbele katika suala hilo. Swali la msingi hapa kwanini makampuni ya kigeni yanaongeza kasi ya kununua ardhi Afrika? Jibu ni biashara.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya ardhi katika Taasisi ya Kimataifa ya Tafiti ya IIED (International Institute for Environment and Development), Lorenzo Cotula kupitia andishi lake la mwaka 2012 la “Land grab or development opportunity?” ambalo lilichapishwa na tovuti ya BBC limesema kuwa ifikapo ifikapo mwaka 2050 idadi ya wamiliki ardhi itapungua lakini wale tuliowaita makabaila ndiyo watakuwa wamiliki wakubwa wa ardhi.

Aidha, ripoti ya Benki ya Dunia ya kati ya mwaka 2011 ilisema uuzaji wa ardhi katika kipindi cha mwaka 2008 na 2009 zaidi ya ekari milioni 60 ziliuzwa. Idadi hiyo ni sawa na theluthi mbili ya ardhi yote ya Afrika.

Ukraine inaongoza kwa upande wa Ulaya, huku Liberia ikiongoza kwa upande wa Afrika kwa kuuza ekari 220,000.

Nchi zinazoongoza kwa uuzaji wa ardhi barani Afrika ni; DR Congo(asilimia 48.8), Msumbiji (asilimia 21.1), Uganda (asilimia 14.6), Zambia(asilimia 8.8), Ethiopia(asilimia 8.2), Madagascar (asilimia 6.7), Malawi (asilimia 6.2), Mali(asilimia 6.1), Senegal (asilimia 5.9), Tanzania (asilimia 5), Sudan (asilimia 2.3), Nigeria (asilimia 1), na Ghana (asilimia 0.6).

Iwapo kwa miaka miwili pekee zaidi ya ekari milioni 60 ziliuzwa, ni ardhi kiasi gani imeuzwa tangu mwaka 2010 hadi leo 2018?

Tuchukue mfano wa Ghana. Wakulima waliofanikisha uzalishaji wa Cocoa kwa wingi kupitia vyama vyao vya ushirika vipatavyo 60,000, ndio maana kwa miaka 20 walifanikiwa kumiliki kampuni zinazozalisha zao hilo kwa asilimia 45 huko Uingereza. Lakini baada ya ardhi yao kuuzwa kwa mwekezaji aliyedai ana mtaji mkubwa wanaishi kwenye wakati mgumu sasa.

Hivyo basi kutokana na mipango hiyo, ekari 100,000 zilinunuliwa, kisha mwekezaji analipia dola moja kwa ekari.

Nini tafsiri yake? Ni kwamba wawekezaji hao wa nje wanatumia vitengo vya uchumi vya Benki ya dunia kuzishawishi taasisi za serikali zetu za Afrika zikubali ushauri, na kuweka unafuu, jambo ambalo tunaliita mazingira mazuri ya uwekezaji.

Mazingira anayoachiwa mkulima wetu ni yale ya kushuhudia kampuni moja ya kigeni inauza madawa, nyingine inakodisha ghala, kisha kuna nyingine inasafirisha mazao yake.

Kampuni nyingine inawekeza kwa kununua ardhi ya mkulima, kisha mkulima anakodi ile ardhi yake kulima zao la kumnufaisha kimaisha.

Je, mkulima huyu atakuwa katika hali gani? Migogoro ya ardhi itakuwa haiishi. Je, kuna tofauti na suala la gesi asilia?

Na suala la gesi asilia limenifanya nikumbuke na kuhofia  kiota cha kuzalisha maandamano na ghasia kupitia ardhi.

Nionavyo, viongozi wetu kabla ya kutoa maamuzi, ni vema ifikie hatua mwekezaji akitaka kununua au kuwekeza katika kilimo wakazi waeneo fulahi angalau asilimia asilimia 50 au asilimia 70 watie sahihi kuwa wamekubali na kama hawatakubali basi waache kumpa mwekezaji, Ushirikishaji wananchi katika maamuzi ni mzuri sana unapunguza migogoro.

Baruapepe; [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles