DK. MASHINJI: MFUMO MPYA WA SIASA UNALIPA

0
942

Na EVANS MAGEGE


KWA wafuatiliaji wa siasa za nchini watakuwa wanamfahamu vyema Dk. Vincet Mashinji.

Mwanasiasa huu kijana liliibuka kwenye siasa za upinzani baada ya kupotea kwa muda mrefu tangu kuibuka kwa migomo ya madaktari nchini enzi za utawala wa awamu ya tatu mwaka 2003.

Dk. Mashinji ni miongoni mwa madaktari waliotimuliwa kutokana na kuongoza mgomo huo ambao ulilenga kuishinikiza Serikali kununua vifaa tiba na madai mbalimbali.

Machi mwaka 2016 Dk. Mashinji aliibuka kwenye siasa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho akirithi kiti hicho kutoka kwa Dk. Willbrod Slaa.

MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano maalumu na kiongozi huyo nakuzungumzia mambo kadha wa kadha  kuhusu mwenendo wa siasa nchini hususani upande wa upinzani.

MTANZANIA Jumapili: Tangu umepata dhamana ya kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, aina ya siasa zako inaonekana kupoa sana kinyume na siasa wazipendazo wana- Chadema, mwenendo huo unamaanisha nini?

Dk. Mashinji: Shughuli za kisiasa mara nyingi huwa ni kutengeneza msukumo wa wananchi katika kufanya shughuli za kimaendeleo, kujiletea maendeleo na kuiacha jamii ikiwa katika utulivu.

Sasa huko nyuma siasa ya hamasa ilikuwa imeutawala zaidi utendaji wa kawaida. Na mazingira hayo unakuta hamasa inameza utaasisi wa taasisi nzima.

Pia baada ya awamu ya tano kuingia madarakani kulikuwa na kitu kinachoitwa  uhalali wa kutawala nchi ambao ulionekana kusumbua.

Hivyo awamu ya tano ikajikuta inafunga midomo watu kwa maana ya kuzuia watu kufanya mikutano ya hadhara na wakosoaji wakubwa wa Serikali wakajikuta wanakumbana vibano vya aina mbalimbali.

Katika mazingira hayo unajikutwa unalazimika kufanya mabadiliko, kwa maana ya kuwa na mfumo mpya wa jinsi ya kuendesha siasa na njia pekee ambayo ilikuwa imeonekana bora zaidi ni kuhakikisha kwamba taasisi inakuwa juu zaidi ya hamasa.

Kwa hiyo hii kubadilisha mfumo wa kitaasisi, mfumo wa wanachama kukaa vikao na kujadiliana kwa kufanya siasa za malengo imelazimishwa na mazingira ya siasa yaliyopo sasa kwamba shughuli za siasa zimekuwa zikipigwa vita sana na Serikali.

Kwa muktadha wa mazingira hayo na hali ngumu za kiuchumi za watu lazima tuje na mfumo ambao unaleta taswira nyingine ambayo ni chanya katika shughuli za kisiasa.

Katika mfumo huo ambao tumeufanya na kuusukuma mbele kwa wananchi matokeo yake unaonyesha unalipa sana.

Ukiangalia kwa asilimia kubwa chaguzi  za marudio katika maeneo ambayo watu wamehamasika kwa maana ya mazingira ya kiuchumi na kielimu yanauafadhali na tumekuwa tunapata kura nyingi.

Pia ukirejea taarifa ya Twaweza kwa siasa hizi ambazo tunazifanya sasa hivi zimekuwa zikishusha ile kukubalika kwa Rais lakini inawezekana kukawa na sababu mbalimbali.

MTANZANIA Jumapili: Pamoja na hiyo taswira ya kisiasa mliyoileta, ukiangalia kwa hizi chaguzi za marudio unaona wazi zinasababishwa na wanachama wenu kuhamia Chama tawala CCM, pia chaguzi zote hizo CCM ndio wanaibuka washindi, sasa mnajipimaje kama mfumo wenu mpya unaodai unalipa?

Dk. Mashinji: Kimsingi CCM hakifanyi shughuli za kisiasa kwa sababu kimeamua kuzikabidhi shughuli zake kwa vyombo vya dola.

Kama CCM ingekuwa inafanya shughuli za kisiasa, kwanza kisingekubali vyombo vya dola kuingilia chaguzi.

Tumeshuhudia polisi wakibandika matokeo, tumeshuhudia mawakala wetu wakilazimishwa na polisi kusaini, tumeshuhudia wakurugenzi wakikataa kupokea fomu za vyama za upinzani.

Kwa hiyo CCM inajua haikubaliki na haiko tayari kwa kufanya shughuli za kisiasa hasa kwenye chaguzi ndio maana wanatumia vyombo vya dola. Na hiyo ni ishara kwamba sisi bado tunakubalika kwa kiasi kikubwa.

Tunaushahidi wa kura ambazo sisi tumepigiwa lakini vyombo vya dola vimetumika kutangaza watu ambao hawakushinda. Mfano Kata ya Sofi kule Malinyi, Tarime, Simuyu, Singida, Momba, Kyera, Mbweni na sehemu mbalimbali.

MTANZANIA Jumapili: Mmeondoka kwenye mfumo wa siasa za hamasa na kuingia katika mfumo mpya wa kusukuma siasa kwa jamii kwa sura ya taasisi, kwanini kuna wimbi kubwa la wanachama wenu wakiwamo viongozi kuhamia chama tawala?

Dk. Mashinji: Kuna sababu mbalimbali zinazowafanya watu kutoka chama kimoja kwenye kingine. Ni kweli hata sisi Chadema  kunawanachama walitoka vyama vingine na kujiunga kwetu.

Ukiangalia makada wetu wengi sana walitoka NCCR – Mageuzi ya kipindi hicho na kilichowafanya makada hao kutoka NCCR kuja Chadema ilikuwa ni sera.

Kwa wakati huo Chadema hakikuwa chama kikubwa kama ilivyo sasa, lakini mfumo wake wa kiuongozi na sera zake ziliwavutia wengi. Na mpaka makada mahili wa CCM walijiunga kwetu.

Kunatofauti kubwa sana kati ya waliohama kutoka vyama vingine kuja Chadema na wale wanaohama kutoka Chadema kwenda vyama vingine.

Kwa hiyo suala la kuhama ni haki ya mtu na hatuwezi kuzuia mtu asihame kwa sababu nchi yetu ni ya kidemokrasia na ni kitu ambacho tumekuwa tunakisema kila siku.

Wanapohama wanatupa changamoto ya kujitathimini na tunagundua kwamba watu wetu wengi wanaohama hawahami kwa utashi wao bali wanahama kwa kushawishiwa, kulazimishwa au kurubuniwa.

MTANZANIA Jumapili: Moja ya sababu za makada wanaohama wanadai ndani ya Chadema hakuna demokrasia, hili likoje?

Dk. Mashinji: Labda tuangalie, hivi unapohama Chadema na kwenda CCM ambacho kinajinasibu kwamba kina wanachama karibu milioni 12, ukiangalia hali ya Jiji la Dar es Salaam na CCM hiyo iliyozalia mwaka 1977 na kukaa madarakani mapaka leo, hivi unaweza ukaamini kwa Jimbo la Ukonga anayeweza kurudisha fomu ni Mwita Waitara peke yake?, Unaweza ukaamini Jimbo la Monduli anayeweza kurudisha fomu Julius Karanga peke yake? Au Jimbo la Siha anaweza akarudisha Mollel peke yake?.

Kwa hiyo unaweza ukabaini huu ni mchezo mchafu na pia una mazingira ya rushwa, mtu anakuja anakubaliana na wewe uende CCM na anakuahidi kukurudishia ubunge wako na lengo lake ni kujaribu kuwahadaa wananchi kwamba wao wanapendwa.

MTANZANIA Jumapili: Unadhani kwa mwenendo huu uliopo kwa makada kuhama kila siku, kwako wewe kama kiongozi unauona mwanga wa kufikia malengo yenu kama chama?

Dk. Mashinji: Kwanza niwaambie tu Watanzania huhitaji watu milioni 20 kuwa wanachama wa chama chako kushinda uchaguzi.

Ndiyo maana sisi kama Chadema hata kwenye mabadiliko ya Katiba kuna vitu ambavyo tulivisapoti kwa mfano awepo mgombea binafsi.

Kwani mgombea binafsi atakuwa na wanachama? Hapana. Chama cha siasa ndani ya Tanzania kina hitaji watu 200 kwa kila mkoa. Kwa hesabu rahisi chama kina hitaji watu kama 4,000 tu  ili kiwe chama cha kudumu.

Kwa hiyo kama chama kinachohitajika ni watu wachache, makada ambao wanauelewa mkubwa juu ya ajenda ya wananchi, makada ambao wako tayari kuzunguka nchi nzima kuelelezea ujumbe wako ambao wananchi watauelewa na kukuchagua na kuunda Serikali.

Inatia huruma sana pale unapoona wananchi wanaambiwa hiki chama kina watu wachache wataundaje Serikali. Kuunda Serikali hakuhitaji watu wengi kwa sababu watumishi wa umma ni watumishi wa watu wote.

Kwa mantiki hiyo Serikali inahitaji watu ambao ni makada wa chama kwa misimamo yetu ni mawaziri, sasa sidhani kama tuna mawaziri 1,000. Wengine wote wanaohitajika ni watumishi wa umma ambao ni Watanzania na wanahaki ya kuunga mkono mtu yeyote.

Kwa msingi huo, katibu mkuu wa wizara haitaji kuwa mwanachama wa chama chochote, mkurugenzi haitaji kuwa na chama chochote, maofisa wa Serikali wakitaka kuwa na vyama ni sawa wakitaka kutokuwa na vyama ni sawa ili mradi wanatekeleza majukumu yao kwa utaratibu uliopangwa.

Watu pekee wanahitaji kuwa wanachama ni wale wenye vyeo vya kisiasa, ambao ni mawaziri wanaounda Serikali.

Kwa hiyo mtu mwenye wasiwasi wa kwamba Chadema haiwezi kuunda Serikali ni yule asiyeelewa mfumo wa utawala wa nchi hii na amelishwa matango pori (propaganda) za CCM na kuaminishwa hivyo.

Pia watu wanaoondoka hawajaanza leo wameanza siku nyingi, katika kumbukumbu alianza akaondoka Katibu Mkuu wa Chadema, Amani Kaburu na wengine wengi mpaka Dk. Slaa.

Kwa hiyo suala la watu kuwa kwenye chama kuhama au kubaki ni suala ambalo limekuwapo lakini kimsingi chama kimekuwa kikiendelea kukua na ukitaka kuona uhai wa chama ni jinsi gani watu wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama au watu wanavyohudhuria vikao vya chama.

MTANZANIA Jumapili: Kuna ukweli wowote kuwa demokrasia ndani ya Chadema inafubazwa na mwenyekiti aliyepo madarakani Freeman Mbowe?

Dk. Mashinji:Kuna kitu kimoja ambacho watu wanatakiwa waelewe, Mbowe si kwamba anajiweka mwenyewe madarakani bali anawekwa na watu, namaanisha anawekwa na ngazi ambazo zimepewa dhamana hiyo.

Kwa utaratibu wa chaguzi za chama chetu mtu anayetaka kugombea kuna kuwa na fomu za kujaza ikimaanisha anaomba kugombea  na anapoomba maana yake anapitiwa na sekretarieti anajadiliwa kisha anapelekwa Kamati Kuu(CC).

CC yetu ina watu wasomi  na wazoefu nao wanakaa na kuchambua kisha kupeleka jina  Baraza Kuu  huko nako unafanyika uchambuzi wa kina kisha jina linapelekwa Mkutano Mkuu. Sasa kweli Mbowe anaweza akajiweka mwenyewe na akapita kweye hatua zote hizo?

Kimsingi chama chochote kinachokwenda kuchagua kiongozi wake kina vitu ambavyo kinahitaji kwa mfano mahitaji ya mtu mwenyewe, uzoefu wake, mazingira ya kisiasa yalivyo kwa hiyo hivi huwa vinangaliwa kwa ukubwa wake ndani ya chama.

Hizi nyingine tunaziona ni propaganda  na kimsingi hata ukipiga hesabu, watu wanadai kwamba Mbowe amezisha muda wa kukaa madarakani. Swali linakuja kwamba Mbowe amezidisha muda wa kukaa madarakani lini na kwanini?.

Kipindi Mbowe anachaguliwa ukiacha mwaka 2014, ukirudi nyuma ukatoa miaka mitano inamaana Mbowe ameiongoza Chadema kwa vipindi vitatu tu, huwezi kusema amezidisha muda na wakati katiba yetu haina ukomo wa mtu kuongoza kiti hicho na wanachama wapo wanaoamua aendelee au asiendelee.

Tuliweka muundo huu kwa sababu chama chetu kilikuwa kinakua, na chama kinapokuwa kilikuwa na watu wachache na viongozi wengi walikuwa anafanya kazi ya kujitolea kukikuza chama lakini baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hapo ndipo hata mimi ninaweza kumpima mtu kwamba ni mwenyekiti wa Chadema.

Kwa sababu tulishinda kwa asilimia 26 ya kura zote ambayo ni robo ya kura zote Tanzania na tulikuwa na uungwaji mkono mkubwa sana. Sasa kwa mtazamo wangu uchaguzi wa kwanza  tunakwenda kumpata mwenyekiti ni ule uchaguzi wa mwaka 2014, kule nyuma alikuwa anajitolea tu kwa sababu alikuwa ni mwenyekiti mtendaji kwa sasa ni mwenyekiti wa chama.

Kwa mantiki hiyo kwa sasa chama kimesamba sana kwa hiyo anaongoza taasisi sio mbaya akawa mwenyekiti  kwa mara nyingine au zaidi yake pia ni ruksa mtu kuwania nafasi yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here