27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Azam yaituliza Bidvest

Pg 32* Yavuna mabao saba, yajibu mapigo kwa Esperance, Twiga stars ‘out’

JENIFER ULEMBO, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Azam jana ilifanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kutamba nyumbani kwa kuichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 4-3 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Azam walifanikiwa kuzima ndoto za wapinzani wao, Bidvest Wits kwa kuwafunga jumla ya mabao 7-3 ikiwa ni ushindi wa mabao 3-0 ugenini na 4-3 nyumbani.

Kwa matokeo hayo, Azam sasa watakutana na timu ngumu ya Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 bora ambao pia juzi walitoa kipigo kikali cha mabao 5-0 kwa timu ya Renaissance ya Chad katika mchezo wa marudiano.

Kwa ushindi ambao Azam imevuna kwa Bidvest Wits ni kama wamejibu mapigo kwa wapinzani wao Esperance ambao pia wamevuka raundi ya kwanza ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 7-0 ikiwa ni ushindi wa 2-0 ugenini na 5-0 nyumbani.

Azam wamefuata nyayo za Yanga ambao juzi walitinga hatua hiyo kwenye Klabu Bingwa Afrika baada ya kuiondosha APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikiwa ni ushindi wa mabao 2-1 ugenini na 1-1 nyumbani.

Matokeo ya ushindi wa Azam jana ulinogeshwa na mabao matatu ‘hat trick’ yaliyopachikwa wavuni na mshambuliaji, Kipre Tchetche, huku moja likifungwa na John Bocco.

Mchezo wa jana ulianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana ambapo Azam ndio walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Bidvest Wits dakika ya 18 kupitia kwa Tchetche aliyemalizia pasi ndefu iliyopigwa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Azam waliendelea kulishambulia lango la wapinzani wao na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 41 kupitia kwa Bocco aliyeunganisha vyema krosi ndefu iliyochongwa na Tchetche.

Bidvest nao walikuja juu na kuandika bao la kwanza dakika ya 44 kupitia kwa Jabulani Shongwe kufuatia makosa ya kizembe yaliyofanywa na mabeki wa Azam.

Azam walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1, lakini waliingia uwanjani kipindi cha pili kwa kasi ambapo Tchetche aliipatia timu yake bao la tatu dakika ya 55 baada ya kuambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kuwazidi mbio mabeki wa Bidvest na kufunga bao hilo.

Dakika ya 58, Bidvest waliandika bao la pili kupitia kwa Koiekantse Mosiatlhaga ambapo dakika moja baadaye alitoka Paseka Sekese na kuingia Mkatshana Luvuyo huku Azam wakimtoa Himid Mao na nafasi yake kuchukuliwa na Jean Mugiraneza.

Azam walifanya tena mabadiliko dakika ya 75 ya kuwatoa Bolou Kipre na Bocco na kuwaingiza Faridi Mussa na Allan Wanga.

Dakika ya 86 Azam walizidi kuwazimisha wapinzani wao kuwa kufunga bao la nne kupitia kwa Tchetche aliyewatoka mabeki na kuambaa na mpira ambapo alimzidi maarifa kipa, Markus Lecki na kuachia shuti lililojaa wavuni.

Wakati huo huo, timu ya soka ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ jana iliondoshwa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Zimbabwe.

Mchezo huo wa marudiano ulichezwa jana katika Uwanja wa Rufaro, uliopo jijini Harare ambapo Twiga Stars wameaga rasmi michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-2, ikiwa ni kipigo cha 2-1 nyumbani na sare ya 1-1 ugenini.

Kikosi cha Twiga Stars kinatarajiwa kurejea nchini kesho mchana kwa usafiri wa ndege ya Shirika la Fastjet.

Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake zinatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Cameroon.

Azam: Aishi Manula, John Bocco, Shamari Kapombe, Ramadhani Singano ‘Messi’, Agrey Morris, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Bolou Kipre, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Kipre Tchetche.

Bidvest: Markus Lecki, Wangu Gome, Maliele Pyle/Jabulani Shongwe, Liam Jordan, Siyabonga Nhlapo, Somila Ntsundwana, Koiekantse Mosiathaga, Onisismor Bhasera, Bongani Khumalo na Paseka Sekese.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles