28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Azam FC yatenga Mil 160 kunasa kifaa cha KCCA

NA MOHAMED KASSARA


KLABU ya Azam FC imetenga kitita cha Dola za Kimarekani 70,000 (Sh Mil 160 za Tanzania) ili kuinasa saini ya kiungo wa KCCA na timu ya Taifa ya Uganda ‘Cranes, Sadam Juma.

Azam imetenga dau hilo ili kuishawishi KCCA kumwachia kiungo huyo fundi na kuongeza nguvu katika chao kinachopigania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Klabu hiyo yenye maskani yake Chamazi, Dar es Salaam, inataka kumsajili Juma ambaye ni mpishi mzuri wa mabao ili kuwafanya washambuliaji wao, Obrey Chirwa na Donald Ngoma, kufunga mabao ya kutosha na kusaidia timu hiyo  kutwaa  ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kurejea katika  michuano ya kimataifa.

Juma ndiye kiungo anayemng’arisha Emmanuel Okwi kwa kumtengenezea pasi za mabao wakiwa Cranes.

Okwi ameifungia Cranes mabao matatu katika michezo minne ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), akitumia pasi za Juma.

Mbali na kumtengeneza pasi za maana Okwi, kiungo huyo alikuwa na mchango mkubwa wakati KCCA ilipowachapa vigogo wa soka la Misri, Al Ahly mabao 2-1, katika mchezo wa makundi  Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela jijini, Kampala, Juma  alifunga bao moja.

Pia aliisaidia Cranes kumaliza nafasi tatu katika michuano ya  Cecafa iliyofanyika mwaka jana nchini Kenya.

 

Lakini Azam  inapigana vikumbo na Simba ambayo pia inamtolea macho  kiungo huyo ambaye anamudu kucheza namba nane na 10.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba, alisema tayari Azam imetenga kitita hicho ili kufanikisha usajili wa mchezaji wake.

“Ni kweli nimepokea ofa Dola 70,000  kutoka Azam ikitaka kumsajili mteja wangu, mchezaji  bado ana mkataba na timu yake, lakini kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka iwapo kuna timu itaweka mezani Dola 80,000 (Sh milioni 180 za Tanzania), tunajaribu kuongea na KCCA kuangalia kama watakubaliana na ofa hiyo.

“Nafahamu kuna ugumu kiasi kwa kuwa KCCA ipo katika michuano ya kimataifa, Juma ni mchezaji mzuri, ukiona Okwi amefunga ujue kazi yote kaifanya yeye, Azam wameonyesha utayari kumsajili, bado tunaendelea na mazungumzo kuangalia kama pande zote zitaridhika na kiasi hicho, lakini mteja wangu hana shida, nataka timu yenye maono ya kufika mbali kama ilivyo Azam, alisema Gakumba, ambaye pia ni meneja wa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles