Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KLABU ya Azam FC inatarajia kuendesha msako wa vipaji kwa vijana walio   chini ya umri wa miaka 17 (U-17) leo katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mpango huo wa kitaifa uliopita kwenye mikoa mingine mitano nchini, utafanyika kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi 9.00 alasiri ndani ya jiji hilo lenye historia ya kutoa wachezaji wengi wenye vipaji waliowahi kutamba na wengine wakitamba hivi sasa nchini.
Mara ya mwisho zoezi hilo lilifanyika jijini Mbeya na kuhudhuriwa na vijana 433, ambapo Azam FC ilivuna vijana 10 pekee watakaoingia kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika mwezi ujao kwenye makao makuu ya Azam Complex, Chamazi.
Mpaka sasa kwenye mikoa yote hiyo, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Dodoma, Zanzibar na Mbeya, Azam FC imechagua jumla ya vijana 60 kati ya vijana 2,999 waliofanyiwa usajili.